Maoni ya wageni

Wagonjwa wanahaki ya kuwajua kwa majina madaktari wanaowatibia – Menejimenti ya hospitali ya MOI.


Na Abdallah Nassoro-MOI.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Pro. Abel Makubi amesema ni haki ya mgonjwa kumjua kwa majina Daktari au Mtalaamu anayemtibia ili kurahisisha mawasiliano juu ya mwenendo wa afya na mpango wake wa matibabu.
Prof. Makubi amesema hayo leo 3 Aprili 2024, wakati wa zoezi la kusikiliza maoni, ushauri, kero, changamoto na pongezi kutoka kwa wateja ambapo amewataka wagonjwa au ndugu wa wagonjwa kuidai haki yao hiyo pale inapokosekana.
“Ni haki yako kumjua Daktari/Mtalaamu anayemtibia mgonjwa wako au anayekutibia, tena kwa majina ili uweze kupata taarifa kutoka kwa mtu sahihi juu ya mwenendo wa matibabu” amesema Prof. Makubi na kunogeza kuwa
“Sisi kama watumishi wa MOI tulishaelekezana hilo, hata hivyo tutaendelea kukumbushana na kulisimamia…unatakiwa kumjua daktari bingwa anayemtibia mgonjwa wako tangu siku ya kwanza unapofika hapa, hii ni haki yako kama mteja wetu.
Amebainisha kuwa maoni mengi yaliyotolewa na wagonjwa au ndugu wa wagonjwa yanaaksi kukosekana kwa muunganiko wa mawasiliano baina ya Watalaamu na mgonjwa au ndugu wa mgonjwa na kwamba amewahimiza watoa huduma kuzingatia jambo hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na rasilimali Watu, Orest Mushi ametoa wito kwa wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya Afya ili kuweza kukidhi gharama za matibabu pindi wanapougua ambapo tayari hadi sasa Serikali inatoa ruzuku katika tiba zao na gharama zingekuwa kubwa mno kwa Wananchi kama Serikali isingefanya hivyo.
Mmoja wa ndugu wa mgonjwa amelalamikia kukosa taarifa za mwenendo wa matibabu ya mgonjwa wake “Nina siku nne hapa MOI, tulipokelewa vizuri na mgonjwa amelazwa ICU lakini sijui kinachoendelea” amesema Juma Namwaka na tayari Muuguzi Mkuu alichukua changamoto hiyo na kufatilia kwani ilionekana changamoto ni mawasiliano/mrejesho kwa ndugu.
Taasisi ya MOI imejiwekea utaratibu wa kusikiliza moja kwa moja maoni ya wateja wake na kutolea ufafanuzi kwa siku za Jumatano na Ijumaa.

About the Author

You may also like these