Rais Samia kugharamia matibabu ya watoto 100 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: Dkt. Samia Suluhu Hassan atagharimia matibabu ya upasuaji na utengamao kwa watoto 100 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi yatakayofanyika katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
 
Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu amebainisha hayo leo Aprili, 21, 2024 alipotembelea Taasisi ya MOI kwa ajili ya kuwajulia hali watoto 25 waliofanyiwa upasuaji chini ya ufadhili wa MO Dewji Foundation.
 
Amesema Rais Dkt. Samia ameguswa na tatizo hilo na ameamua kugharamia matibabu ya watoto 100 zaidi ili kuepusha madhara na ulemavu unaoweza kusababishwa na kuchelewa kufanyiwa upasuaji.
 
“Nimemsikia mwenyekiti wa chama cha wazazi na walezi  wenye watoto wa tatizo hili la kichwa kikubwa na mgongo wazi kwamba wana watoto kama 200 wanaopaswa kufanyiwa upasuaji lakini wazazi hawana uwezo….
 
Mheshimiwa Rais Samia amenielekeza, nilete pesa kwa ajili ya watoto 100 ambao watafanyiwa upasuaji  wa kichwa kikubwa na mgongo wazi  bure kwa gharama za Rais Samia  Suluhu Hassan.
 
Kwa hiyo Prof. Makubi wasilianeni na ASBATH kujua watoto hawa ndani ya wiki moja mbili wizara italeta hizo fedha za kugharamia matibabu au upasuaji na huduma za utengamao kwa watoto 100 kutoka kwa Rais wetu Mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan” amesema Waziri Ummy
 
Aidha Waziri Ummy ameipongea taasisi ya MOI kwa kutoa matibabu ya watoto hao na MO Dewji Foundation kwa ufadhili wa matibabu ya watoto 50, huku akiwataka wadau kuendelea kujitokeza kusaidia wengine.
 
“Kubwa nataka kutoa wito kwa wazazi wenzangu kwa wale wenye watoto wenye changamoto hii ya vichwa vikubwa na mgongo wazi wasiwafiche watoto hao, wahakikishe wanapeleka kliniki ili wapate ushauri wa kitaalam” amesema Waziri   na kusisistiza kuwa
 
Kwa upande wake daktari bingwa mbobezi wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu MOI, Dkt. Hamisi Shabani amesema tatizo la vichwa vikubwa linaweza kuzuilika kwa kuhakikisha wanaume wanawalisha wake zao vyakula vyenye madini ya Frolic Acid na kuwawahisha kliniki kwa wale wenye tatizo hilo.
 
Mkurugenzi wa MO Dewji Foundation Imran Sherali ameishukuru serikali na taasisi ya MOI kwa kufanikisha matibabu hayo na kuongeza kuwa taasisi hiyo ipo tayari uendelea utoa msaada kwa watoto wengine.
 
Naye mwenyekiti wa chama cha wazazi na walezi wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Tanzania (ASBATH) Norbert Kyando amesema kwa sasa chama hicho ina orodha ya watoto 200 wanaohitaji matibabu lakini kutokana na ukosefu wa fedha wapo majumbani huku wachache wakihudhuria klinik za watoto wa matatizo haya.

About the Author

You may also like these