Rais wa Somalia atembelea MOI kuona huduma za kibingwa na kibobezi za tiba ya mifupa na ubongo.


Na Abdallah Nassoro-MOI
Rais wa Jamhuri ya Somalia Mheshimiwa Dkt. Hassan Sheikh Mohamud leo Aprili, 27, 2024 ametembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kujionea huduma za kibingwa na kibobezi za tiba ya mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu zinazotolewa katika taasisi hiyo.

Sambamba na hilo Rais Dkt. Mohamud amesema serikali yake ipo tayari kuwaleta wananchi wake wenye matatizo ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu MOI kwa matibabu ya kibingwa na kibobezi na pia kuwaleta madaktari wanafunzi kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo (intern).

Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu (MB) amesema ziara hiyo imelenga kuanzisha ushirikiano katika sekta ya afya kwenye eneo la tiba za kibingwa na kibobezi.

“Kama mnavyofahamu nchini yetu imepiga hatua kubwa katika eneo hilo, tunao wataalam bingwa na bobezi katika hospitali zetu za JKCI, Muhimbili na Taasisi ya MOI” amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Prof. Abel Makubi amesema ziara hiyo imejenga misingi ya ushirikiano baina ya taifa hilo na MOI kupitia wizara ya afya katika maeneo ya kutoa tiba za kibingwa na kibobezi kwa wananchi wa Somalia, madaktari wanafunzi na tafiti za kisayansi .
“Ujio wa Rais Mohamud umelenga kuboresha ushirikiano katika tiba utalii ambapo MOI ina uwezo mkubwa kupitia wataalam wake kutokana na uwekezaji uliofanywa na serikali yetu hapa MOI, tutatoa tiba ya mifupa na ubongo pamoja na ajali kwa raia wanaotoka Somalia

…sisi tumemuahidi tupo tayari kwenda kuwahudumia wananchi wa Somalia wanapotuhitaji na kuwajenga uwezo katika hilo eneo” amesema Prof. Makubi na kuongeza
“Tupo tayari pia katika kushirikiana nao kuwapa mafunzo katika ngazi ya Shahada ya Uzamili na madaktari wanafunzi kuja kupata mafunzo kwa vitendo (Intern) wanaokuja kwenye (Intern), vilevile kwa wale ambao wanataka kuongeza uzoefu katika Tiba ya Mifupa na Ubongo”

Aidha Prof. Makubi amesema sehemu nyingine ya ushirikiano ni pamoja na kufanya tafiti za kisayansi za kitabibu ambazo zitaleta tija kwa wananchi wa Somalia na Tanzania

About the Author

You may also like these