Watoto 50 wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi wafanyiwa upasuaji MOI


Na Abdallah Nassoro-MOI
Watoto 25 wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi wamefanyiwa upasuaji leo Jumamosi Mei, 4, 2024 katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na kutimiza idadi ya watoto 50 waliopata matibabu hayo chini ya ufadhili wa MO Dewji Foundation.

Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa taasisi ya MOI, Dkt. Hamisi Shabani amesema upasuaji wa watoto wote 50 umefanyika kwa mafanikio makubwa na kwamba watoto 25 waliofanyiwa upasuaji awali hali zao zinaendelea vizuri.

“Leo tumekamilisha upasuaji wa watoto 25 waliobakia ili kutimiza watoto 50 ambao wamefadhiliwa na taasisi ya MO Dewji Foundation, watoto 25 wa kwanza tuliowafanyia upasuaji wiki iliyopita wanaendelea vizuri…tunaishukuru sana MO Dewji Foundation kwa ufadhili huu” amesema Dkt. Shabani na kuongeza kuwa

“Pia tunamshukuru Mheshimwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ufadhili wa matibabu ya watoto wengine 100, pia tunamshukuru Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kuja kuwajulia hali watoto hawa na mwisho nimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wetu wa MOI kwa jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya matibabu ya watoto wengine 100 kupitia MOI Marathon msimu 2024”

Kwa upande wake muuguzi Pezania Selege amesema watoto wote waliofanyiwa upasuaji katika kambi ya awali wanaendelea vizuri na tayari waliruhusiwa kurejea nyumbani kwao na kwa sasa wanahudhuria kliniki.

“Maendeleo ya watoto wetu ni mazuri na tayari tumewaruhusu kurudi nyumbani na kwasasa wanahudhuria kliniki, upasuaji wa leo umetimiza jumla ya watoto 50 waliofanyiwa upasuaji katika kambi hizi mbili, naishukuru MO Dewji Foundation kwa kuwajali watoto hawa”

Mbio za MOI marathon zinatarajia kufanyia Juni 30, 2024 ambapo kaulimbiu ni kuchangia matibabu ya watoto 100 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

About the Author

You may also like these