Watumishi MOI wahimizwa kuelewa umuhimu wa ukaguzi na kuwapa ushirikiano wakaguzi


Na Abdulaziz Seif-MOI
Watumishi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamepatiwa mafunzo elekezi ya kuelewa umuhimu wa ukaguzi, taratibu za ukaguzi na kuboresha uhusiano na waakaguzi wa ndani na wa nje ili kuiwezesha taasisi kuboresha huduma na kufikia malengo yake kupitia utekelezaji wa hoja na mapendekezo yanayotolewa na waakaguzi.
Meneja wa Ukaguzi wa Ndani wa Taasisi ya MOI, CPA Flora K. Masami amesema hayo leo Alhamisi Mei, 9, 2024 wakati wa mafunzo hayo kuwa, baadhi ya watumishi wamekuwa wakiona wakaguzi kama sehemu ya mashtaka kwao na hivyo kutoa ushirikiano hafifu wakati wakaguzi wanapotekeleza majumu yao.
CPA Masami amebainisha kuwa watumishi hawana sababu ya kuhofia ukaguzi kwa sababu upo kwa ajili ya kuiwezesha taasisi kufikia malengo yake na kwamba ukaguzi wa kawaida unalenga kubaini sehemu zenye changamoto ili kuzifanyia maboresho.
“Suala la kutafuta makosa halipo katika ukaguzi wa kawaida, tunakuja kuangalia namna unavyofikia malengo, namna tunavyozingatia sheria na taratibu, kama kuna mifumo ya udhibiti na kama kuna vihatarishi vya kushindwa kufikia malengo…Kama zikibainika changamoto tunashauri namna ya kurekebisha hizo changamoto, sisi tupo ili kuisaidia taasisi kufikia malengo” amesema CPA Masami
Amesisitiza kuwa hoja inapotolewa, wakaguliwa wanapaswa kujielekeza kutekeleza kilichopendekezwa, ili kuponya visababishi vya hilo tatizo, kudhibiti vihatarishi na madhara hasi yanayoweza kutokea badala ya kujitetea, au kuwatupia mpira wengine na kwamba mwenye jukumu la kujibu hoja au kutekeleza hoja ni yule mmwenye kusimamia eneo husika si vinginevyo.
Amewaomba watumishi wote kujiandaa kwa ajili ya ukaguzi ujao wa CAG wakati tukiendelea kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa kwenye kaguzi za nyuma na wakaguzi wote wa ndani na wa nje.

About the Author

You may also like these