Tanzania kuwa kitovu cha tiba utalii

Na. WAF – Dar es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Tanzania inakwenda kuwa kitovu cha Tiba Utalii kwa kutoa huduma za Afya kwa wagonjwa maalumu wa ndani na nje ya nje.

Waziri Ummy amesema hayo leo Novemba 28, 2023 baada ya kufungua mradi wa kliniki mpya ya wagonjwa maalum na wa kimataifa iliyopo katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) itakayotoa huduma za kliniki kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi.

“Haya tutakayoyashuhudia leo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa ambao Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya katika Sekta ya Afya lakini pia niwapongeze Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) chini ya Prof. Abel Makubi na Mwenyekiti wa Bodi Prof. Charles Mkony kwa kazi nzuri na kubwa ya kuokoa maisha ya Watanzania”. Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amewaomba Watanzania wenye uhitaji wa tiba kwa haraka (kliniki ya wagonjwa maalum na Wakimataifa) ikiwa ni mtumishi au mfanyabiashara waende MOI ambapo ndani ya masaa mawili unamaliza kila kitu na kuendelea na shughuli zako.

Aidha, Waziri Ummy ameitaka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) iendeshe kliniki hiyo mpya ya wagonjwa maalum na wa kimataifa kwa ubia na wawekezaji wengine ili kuboresha zaidi huduma zitolewazo.

“Ni jambo zuri sana mmelianzisha lakini tusije kukwama njiani hivyo tushirikiane na wadau wengine ili huduma hii iendelee na ni matarajio yangu kwamba kliniki hii mpya ya wagonjwa maalumu na wagonjwa wa Kimataifa itakuwa kliniki ya mfano ambayo itakua kivutio kikubwa kwa wagonjwa kutoka katika Mataifa mbalimbali”. Amesema Waziri Ummy.

Amesema, Kutokana na uwekezaji mkubwa katika miundombinu vifaa tiba na wataalamu, Taasisi ya MOl imefanikiwa kupunguza rufaa za wagonjuwa kwenda nje ya nchi ambapo hivi sasa 99% ya huduma za mifupa zinapatikana hapa nchini na 97% ya huduma za kibingwa za Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Gahamu zinapatikana hapa chini.

Pia, Waziri Ummy ametoa maelekezo kwa Hospitali nyingine kuwa na huduma za haraka kwa kuwa Watanzania wanataka huduma za haraka na zilizobora kwa kuzingatia Weledi, Maadili na Taaluma wakati wa kumhudumia mgonjwa kwa kuanza na mapokezi mazuri.

Waziri Ummy amewataka Watanzania kuzingatia ulaji bora ikiwemo kupunguza matumizi ya sukari nyingi, chumvi nyingi pamoja na mafuta mengi ili kuepuka Magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la juu la Damu (Presha) na Kisukari kwa kuwa magonjwa hayo yamekuwa yakiongezeka Tanzania.

Mwisho, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio cha Watanzania na kuboreha huduma za Afya ikiwemo kutoa fedha kwaajili ya majengo, vifaa na vifaa tiba na Sasa tunakwenda kuwa kitovu cha Tiba Utalii.

About the Author

You may also like these