Madaktari bingwa wa MOI kutoa huduma za mifupa na ubongo katika Melivita ya Jeshi la ukombozi la watu wa China.

Na Abdallah Nassoro-MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) itashirikiana na madaktari bingwa wa Melivita ya matibabu ya Peace Ark ya Jeshi la Ukombozi la watu wa China kutoa matibabu ya kibingwa na kibobezi ya mifupa na ubongo wakati wa kambi maalum ya matibabu ya jeshi hilo nchini.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Lemeri Mchome amesema leo Julai, 16, 2024 baada ya timu ya wataalam kutoka Jeshi la ukombozi la watu wa China kutembelea Taasisi ya MOI, kuwa madaktari wake wapo tayari kushirikiana kutoa matibabu ya kibingwa na kibobezi bure kwa wananchi ikiwa pamoja na upasuaji.

“MOI ndiyo kituo cha umahiri cha matibabu ya kibingwa na kibobezi ya mifupa, nyonga, mgongo, kiuno, ubongo na mishipa ya fahamu…sisi kama Taasisi tupo tayari kushirikiana nanyi kwenye kutoa matibabu katika vyumba vyetu vya upasuaji na kule kwenye meli” amesema Dkt. Lemeri

Kwa upande wake Luteni Kanali wa Jeshi la Wananchi Tanzania Dkt. Pius Horumpende amesema ziara hiyo imelenga kuwatambulisha watoa huduma hao na kwamba wanatarajia kushirikiana katika upasuaji wa mifupa ubongo na mifupa ya fahamu.

Naye kiongozi wa timu hiyo, Naibu Kamanda Tong Tao ameshukuru kwa mapokezi na kwamba anataraji zoezi hilo litafanyika kwa ufanisi mkubwa.
Meli hiyo itakuwepo chini kutoa huduma za kitabibu bure kuanzia tarehe 16 Julai, 2024 hadi tarehe 23 Julai, 2024 ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka sitini (60) ya ushirikiano kati ya Tanzania na China na Maadhimisho ya Miaka Sitini (60) tangu kuanzishwa kwa JWTZ tarehe 01 Septemba, 1964.

About the Author

You may also like these