Na Abdallah Nassoro-Sabasaba
Jumla ya wananchi 1,436 wamepatiwa huduma za matibabu ya kibingwa ya mifupa, mgongo, nyonga, magoti, ubongo, mishipa ya fahamu, mazoezi tiba na lishe katika banda la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwenye maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa ya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Lemeri Mchome amesema ushiriki wa taasisi hiyo katika maonesho hayo umelenga kusogeza karibu na wananchi huduma za kibingwa na kutoa elimu ya kujikinga na tabia hatarishi kwa afya ya mifupa na ubongo.
“Kwa ujumla tumehudumia watu 1,432 kati ya hao watu 432 wamepewa rufaa ya kwenda katika taasisi hiyo kwa matibabu zaidi, watu 700 wamepata vipimo bure vya uzito, urefu, sukari, shinikizo la damu na ushauri wa lishe bora, watu 300 wamepata matibabu ya mazoezi tiba na watu 245 wamepima bure katika kipimo cha “Ultra Sound”” amesema Dkt. Lemeri
Ameongeza kuwa “Tumetoa huduma hizi bure ili wananchi wengi waweze kupata matibabu ya kibingwa na kibobezi, huduma kama hizi walipaswa kuzilipia lakini tukasema hapana waache wananchi wengi wafaidike na huduma zetu za kibingwa na kibobezi”
Kaimu Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa wananchi wenye matatizo ya mifupa, nyonga, mgongo, kiuno, ubongo na mishipa ya fahamu kufika MOI kwa matibabu ya kibingwa na kibobezi .
