MOI ipo tayari kutoa matibabu ya kibingwa kwa wanamichezo AFCON

Na Abdallah Nassoro-MOI

Taasisi ya tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeendesha kambi ya bure ya uchunguzi wa kibingwa wa maumivu ya magoti kwa wanamichezo na wananchi wa kawaida ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kutoa matibabu ya aina hiyo kwa wanamichezo wakati wa mashindano ya AFCON mwaka 2027 ambapo Tanzania itakuwa moja ya nchi mwenyeji.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Lemeri Mchome akizungumza na wagonjwa walioudhuria katika kambi hiyo leo Julai,18, 2024 amesema taasisi hii ya wananchi, imejipanga kutoa matibabu kwa wanamichezo na kwamba kambi hiyo ni sehemu ya maandlizi hayo.

“MOI ndiyo taasisi ya Kitaifa yenye madaktari bingwa na bobezi wa matibabu ya mifupa na viungo ikiwemo magoti, kuelekea AFCON 2027 ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji tumejipanga kuwapatia tiba sahihi za kibingwa katika hadhi ya kimataifa wanamichezo watakaopata majeraha magoti na viungo” amesema Dkt. Mchome

Amefafanua kuwa kambi hiyo ya uchunguzi wa magoti bure kwa wanamichezo ilikuwa ya siku moja ila kutokana na maombi ya wagonjwa ameiongezea siku moja zaidi, ili wanamichezo na wananchi wengi waweze kupata huduma hizo.

“Baada ya kambi hii tutajipanga kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi ambao wanashindwa kupata matibabu ya kibingwa kutokana na umbali pia na kutokuwa na uwezo wa kufika MOI” amebainisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo.

Kwa upande wao wagonjwa waliofika kupata matibabu hayo wameipongeza menejimenti ya MOI kwa kambi hiyo na kuomba kujenga utamaduni wa kuwa na kambi nyingi za aina hiyo ili wananchi wengi wafikiwe na huduma za kibingwa.
“Niupongeze uongozi kwa kubuni hili na pia kwa mkurugenzi kuja kutusalimia, hii inaonesha mnaweka mbele maslahi ya wananchi, hongereni sana” amesema Abdallah Ausi.
Mmoja wa waratibu wa kambi hiyo daktari bingwa wa mifupa Dkt. Joseph Sabas amesema zaidi ya wagonjwa 150 wakiwemo wanamichezo wametibiwa na wengi wao wakiwa na majeraha ya magoti yanayotokana na shughuli wanazofanya.

Kambi hizi zitakuwa endelevu kuhakikisha MOI inaleta mchango katika tasnia ya michezo lakini pia na wananchi wengine wasio wanamichezo watapata fursa ya kupata uchunguzi na ushauri ikiwemo na tiba.

About the Author

You may also like these