MOI kudumisha ushirikiano na Chuo cha Colorado Marekani

Na Mwandishi Wetu-MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imesema itadumisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Colorado cha nchini Marekani kuendelea kuwajengea uwezo na umahiri madaktari wazawa kufanya upasuaji uvimbe wa ndani ya ubongo, ikiwa ni muendelezo wa jitihada za taasisi za kuboresha utoaji wa huduma za kibobezi kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa leo Februari, 23, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof Abel Makubi wakati akifunga mkutano wa tatu wa kimataifa wa upasuaji wa ubongo kwa njia ya matundu madogo ili kuondoa uvimbe wa ndani ambapo amekishukuru hicho chuo kwa jitihada zake kuwajengea uwezo madaktari wazawa ili wawe mahiri katika tiba hiyo.

“MOI inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na Chuo Kikuu cha Colorado Marekani, ushirikiano huu wenye faida kubwa kwetu, ni miaka 11 tangu kuasisiwa kwa program hii, nampongeza Prof. Joseph Kahamba kwa kuasisi program hii ambayo leo inakwenda kuwajengea uwezo vijana wetu” amesema Prof. Makubi na kuongeza kuwa

“Tunashukuru pia kwa msaada wenu wa kifaa cha kufanyia upasuaji huo chenye thamani ya Tsh. 200 milioni, niwahakikishie kuwa sisi MOI tutasimamia matumizi na utunzaji sahihi wa kifaa hiki ili kidumu na kutoa huduma kwa wagonjwa wengi”

Awali Mkurugenzi wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa Taasisi ya MOI Dkt. Lemeri Mchome amesema watalaam wa MOI wametumia muda wa mkutano huo pia kukamilisha mtaala huo na kuuwasilisha Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya uthibitisho.

“Tumeshirikiana na wenzetu hawa kuandaa mtaala wa kufundishia kozi ya matibabu ya ubongo, kwasasa mtaala huo upo TCU na tunatarajia mwakani tunaweza kupokea wanafunzi wa kozi hii mpya” amesema Mchome

Kwa upande wake Prof. Ryan Ormond kutoka chuo Kikuu cha Colorado Marekani amesema programu hiyo inayolenga kuwajengea umahiri wataalam wa MOI kufanya upasuaji wa kuondoa uvimbe sehemu ya ndani ya ubongo, sambamba na huduma bora za kibobezi za uuguzi.

Mratibu wa mafunzo hayo daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo kwa watoto Dkt. Nicephorus Rutabasigwa amesema mkutano huo wa siku tano umewezesha upasuaji wa watoto Sita kwa mafanikio makubwa, wakati wengine watatu wakitarajiwa kufanyiwa upasuaji huo na kufikia idadi ya wagonjwa Tisa.

Neema Roy ni Muunguzi Mbobezi kutoka hospitali ya Rufaa Mbeya amesema mafunzo hayo yamemjengea uwezo wa kutambua umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano baina ya madaktari, wauguzi na wataalam wengine wanaohusika katika mnyororo huo.

About the Author

You may also like these