Na Mwandishi wetu- MOI
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Ukimwi leo 22/02/2024 imetembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili MOI kwa lengo la kukagua maeneo mbalimbali ya kutolea huduma kwa wananchi.
Kamati hiyo ikiongozwa na makamu mwenyekiti wake Dkt. Faustine Ndugulile imetembelea kitengo cha radiolojia, jengo la kisasa la kusubiria wateja (Clients Lounge) Kliniki mpya ya wagonjwa maalum na wakimataifa (Premier and International patient services) pamoja na wodi za kulaza wagonjwa.
Akifanya majumuhisho ya ziara hiyo Dkt.Ndugulile ameipongeza Taasisi ya MOI kwa maboresho makubwa iliyoyafanya ndani ya kipindi kifupi chini ya uongozi wa Prof. Abel Makubi.
“Tunaipongeza MOI, hongereni sana Mkurugenzi mko katika muelekeo sahihi, hongera sana kwa mwenendo mnaokwenda nao ni mzuri, kamati inawapongeza ,kamati ya Bunge imeridhika na sisi tutakuwa mabalozi” alisema Dkt. Ndugulile. Aidha, Makamu Mwenyekiti amewaasa watendaji wote wa MOI kubadilika(adapt) katika utendaji na kujipanga pamoja na Mkurugenzi katika dira moja ya kuwajibika kwa matokeo.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Afya Dkt. Mollel(MB) amewataka watumishi wa MOI kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuendana na mabadiliko chanya yaliyopo, pia ameahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yote ya kamati. Aidha, amewataka watumishi wote kutokufanya kazi kwa mazoa na ni lazima wakubali kujitoa zaidi na kuacha mambo ambayo hayaleti uwajibikaji kwa Wananchi.
Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji wa MOI Mkurugenzi mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi amesema kutokana na uwekezaji uliofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi zimepungua kwa asilimia 99% kwa wagonjwa wa mifupa na asilimia 97% kwa wagonjwa wa Ubongo na mgongo.