Kamati ya kudumu ya Bunge ya afya na UKIMWI yashauri kuanzishwa kwa Taasisi ya sayansi na neorolojia

Na Mwandishi Wetu-MOI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI imeishauri Wizara ya Afya kutekeleza mambo Sita muhimu ili kuboresha utoaji wa huduma katika Taasisi ya Tiba na Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na taasisi zingine.

Ushauri huo umetolewa leo Februari 22, 2024 ilipofanya ziara katika Taasisi ya MOI kuona hali ya utoaji wa huduma.

Akizungumza wakati wa majumuisho Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt. Faustine Ndungulile amesema ushauri wa kamati ni pamoja na uanzishwaji wa mfuko wa Vipandikizi (implant Fund) ili kukabiliana na gharama kubwa ya vifaa hivyo kwa Wananchi.

Amesema gharama za vipandikizi ni kubwa na kwamba wananchi wengi wanashindwa kumudu na hivyo kusababisha MOI kubeba mzigo huo kitu ambacho kitasababisha huduma kukosa mzunguko wa vifaa .

Pia kamati hiyo imeishauri MOI na Wizara ya Afya kuweka mipango ya upanuzi wa Hospitali hiyo ili iweze kukidhi mahitaji ya sasa ambapo idadi ya wagonjwa ni kubwa ikilinganishwa na eneo lililopo hivyo kusababisha msongamano wa wagonjwa .

Dkt. Ndungulile pia amesema kuelekea mashindano ya AFCON yajayo ambayo Tanzania ni mwenyeji ni muhimu kwa taasisi hiyo ijipange kutoa huduma bora kwa Wanamichezo.

“MOI ijipange vyema kwa ajili ya AFCON katika ubora wahuduma kwa majeruhi hasa wanamichezo” amesema Dkt. Ndungulile

Kuhusu mfuko wa bima ya afya kutoa bei ndogo kwa huduma za vipandikizi kamati hiyo imeiagiza Wizara ya Afya izikutanishe MOI, JKCI , MNH na NHIF , MSD ili kuangalia uhalisi wa bei za za baadhi ya huduma kama hizi zinazohitaji vipandikizi.

Aidha imeiagiza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ishirikishe MOI na JKCI katika mradi mkubwa wa kuijenga upya MNH .

Ushauri mwingine wa kamati hiyo ni pamoja na Wizara ya Afya kuiwezesha MOI kuwa na Taasisi ya Tiba ya magonjwa ya ubongo ma mifumo ya fahamu(Neuroscience Institute) ambayo itajikita katika Huduma zote za upasuaji na tiba ya kawaida

Pia kamati imeipongeza MOI kwa kuboresha huduma za matibabu ya mifupa, Ubongo,mgongo na mishipa ya fahamu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Wizara imeyapokea maelekezo na ushauri wa kamati na itayakanyia kazi kwa ustawi wa sekta ya afya nchini.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi aliishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwekeza shillingi billion 5 katika mitambo ya uchunguzi ya MRI , CT na vifaa vya wagonjwa mahututi na dharura.

About the Author

You may also like these