Na Stanley Mwalongo- MOI
Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Patrick Mvungi amewaasa wananchi kujiunga na bima ya afya ili iwasaidie kupata matibabu hospitalini pindi watakapougua.
Mvungi ameyasema hayo leo Februari 14, 2024 wakati wa zoezi la kusikiliza na kupokea maoni, changamoto, kero na pongezi kutoka kwa wateja wa taasisi hiyo katika banda la kusubiri wagonjwa na kusisitiza kuwa Serikali imepitisha mswada wa bima ya afya kwa wote hivyo watanzania watafute utaratibu mzuri wa kujiunga na bima ya afya.
“Niwaombe mjiunge na bima ya afya ukiwa na bima ya afya itakusaidia katika maeneo mengi, ugonjwa hauna taarifa huwa unakuja ghafla ukiwa na bima ya afya itakusaidia usitumie pesa taslim……Serikali imepitisha mswada wa bima ya afya kwa wote kwahiyo niwaombe watanzania wenzangu tafuteni utaratibu mzuri mjiunge na bima ya afya zitawasaidia” amesema Mvungi.
Pia amewasisitiza wateja wa Taasisi ya MOI wasisite kupiga simu au kutuma ujumbe kwa viongozi wa Taasisi hiyo kupitia namba za viongozi hao ambazo zipo kwenye mabango yaliopo katika maeneo mbalimbali MOI pindi wanapopata changamoto yoyote.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi MOI Sr Judith Ndege akijibu pendekezo la mteja aliyeshauri wazee wapewe kiupaumbe kwenye matibabu amesema MOI inautaratibu wa kuwapa kipaumbele makundi maalum ambao ni watoto, wasiojiweza na wazee pindi wanapotibiwa katika taasisi hiyo.
Naye ndugu wa mgonjwa Mika Henry ameupongeza uongozi wa Taasisi ya MOI katika nyanja zote kuanzia chini mpaka juu kwa huduma bora na kusisitiza kuwa ni Mungu pekee atawalipa watumishi wa MOI kwa kazi nzuri wanayofanya.
Menejimenti ya MOI imekuwa na utaratibu wa kupokea maoni, changamoto, kero na pongezi kutoka kwa wateja wake kila siku ya jumatano na ijumaa kwa lengo la kuboresha huduma za MOI.