Na Amani Nsello- MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imepokea msaada wa runinga Sita kutoka Kampuni ya Ving’amuzi ya Azam Tv wakishirikiana na kampuni ya vifaa vya kielekitriniki Mr UK.
Akipokea msaada huo leo Alhamis Machi 6, 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amezishukuru kampuni hizo kwa kutoa msaada huo kutoka sehemu ya faida wanayoipata katika biashara zao.
“Tunawashukuru sana Azam na Mr UK kwa kazi nzuri, kwa kutambua kwamba katika faida wanayoipata katika biashara wanarudisha kwa jamii hiyo hiyo” amesema Dkt. Mpoki
Dkt. Mpoki amesema kuwa runinga hizo zitawasaidia wagonjwa kuweza kupata taarifa mbalimbali wakati wakiendelea kupatiwa matibabu katika taasisi hiyo.
Mkurugenzi Huduma za Uuguzi wa MOI, Fidelis Minja ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kutoa misaada mbalimbali katika taasisi hiyo ikiwamo vifaa vya ukarabati wa jengo na miundombinu mingine.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mr UK, Shedrack Theophil amesema kuwa sio mara yao ya kwanza kutoa msaada wa aina hiyo na wataendelea kushirikiana na MOI kwa ajili ya kuwa sehemu ya kurudisha faraja kwa wagonjwa.