Wanawake MOI wafadhili upasuaji wa watoto wanne wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi

Na Amani Nsello- MOI

Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kesho Machi 8, 2025 Watumishi wanawake wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamefadhili upasuaji kwa watoto wanne wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo.

Mwenyekiti Wanawake TUGHE MOI, Elizabeth Mrindoko amebainisha hayo leo Ijumaa Machi, 7, 2025 katika hafla fupi ya kuelekea kilele cha sherehe hizo iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano MOI.

Bi. Elizabeth amesema kuwa lengo lao lilikuwa ni kufanikisha matibabu ya watoto 10 wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi lakini mpaka sasa wamewezesha watoto 4 kufanyiwa upasuaji kwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya na kuomba wadau wengine wajitokeze kuwasaidia watoto hao.

” Hadi leo ninavyozungumza hapa tumefanikisha matibabu ya watoto wanne, wanawake MOI kwa kushirikiana na wadau kama Nyota Foundation, Madina Foudation, TAKUKURU, Kauthar, Samba Store, NHIF_ Kinondoni, Zia Sia Family, KAUTHAR, Road Safety Ambassador of Tanzania (RSA), Tema Traders, hivyo tunaomba pia wadau wengine wajitokeze ili tufanikishe lengo letu la kutibu watoto 10″- amesema Bi. Elizabeth

Aidha, Bi. Elizabeth ameongeza kuwa wanawake hao wa MOI na wadau wametoa msaada wa vifaa tiba, viti mwendo sita, sabuni za kufulia, taulo za kike, pampasi, sukari, dawa za meno.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa MOI, Dkt. Asha Abdullah amewaasa wanawake hao kuzingatia maadili wakati wakitimiza majukumu yao hususani mavazi na kuendeleza umoja na mshikamano kwani ndiyo msingi wa mafanikio katika maisha.

About the Author

You may also like these