Mamia wajitokeza kuchangia damu MOI katika maadhimisho ya siku ya mchangiaji damu duniani

Na Mwandishi wetu- MOI

Zaidi ya Wanafunzi 400 kutoka katika Shule na Vyuo mbali mbali Dar es Salaam leo wamejitokeza kuchangia damu katika Taasisi ya MOI katika maadhimisho ya siku ya mchangiaji damu duniani.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Prof. Abel Makubi amewashukuru wachangiaji damu wote waliojitokeza kuchangia damu kwani mahitaji ya damu katika Taasisi ya MOI ni chupa 15 mpaka 30 kwa siku.

Prof. Makubi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kuchangia damu kwani hakuna kiwanda cha kutengeneza damu na wala haiuzwi hivyo lazima damu itoke kwa binadamu mwingine

“Pia, nitumie fursa hii kuwaelekeza watumishi wote wa MOI kwamba damu haiuzwi hivyo mgonjwa yeyote anayeitaji damu asije akauziwa damu kwani wachangiaji damu wanachangia bure na Serikali inagharamia upimwaji wa damu hiyo.” alisema Prof. Makubi

Naye Mdau wa afya na Mfanyabiashara Azim Dewji amesema anatambua umuhimu wa uchangiaji damu kwani hakuna kiwanda cha damu na ni lazima damu itoke kwa binadamu mwingine.

“Tumekuwa tukishirikiana na Taasisi ya MOI katika matukio mbalimbali ya uchangiaji damu kwa kushirikiana na timu za Simba na Yanga ambapo chupa zilizopatikana tunaamini zimesaidia kuokoa Maisha ya wagonjwa” Alisema Azim Dewj

Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi ametoa vyeti kwa shukrani kwa Taasisi, Vyuo pamoja na wadau mbalimbali ambao wamekua wakishiriki katika mazoezi ya uchangiaji damu katika Taasisi ya MOI.

About the Author

You may also like these