Prof. Makubi akabidhiwa ofisi rasmi na kuanza majukumu MOI.

Na Mwandishi wetu- MOI

Mkurugenzi mtendaji mpya wa Taasisi ya tiba ya mifupa Muhimbili (MOI) Prof. Abel N. Makubi amekabiziwa ofisi na mkurugenzi mtendaji aliyemaliza muda wake Dkt. Respicious Boniface na kuanza majukumu yake rasmi.

Akizungumza wakati wa makabiziano Prof. Makubi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kuisimamia Taasisi muhimu ya MOI ili kuendelea kuboresha huduma za kibingwa za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kwa wananchi.

“Kwa namna ya pekee nimshukuru sana Waziri wa Afya Mh Ummy Mwalimu (MB) Naibu Waziri, Katibu mkuu Wizara ya Afya, Mganga mkuu wa Serikali pamoja na viongozi wengine wa Wizara kwa kuendelea kuisimamia vyema sekta ya afya hapa nchini” Alisema Prof. Makubi.

Kwa upande mwingine, Prof. Makubi ameomba ushirikiano wa dhati kwa menejimenti na watumishi wote wa MOI ili kuhakikisha azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya inatekelezwa.

“Wana MOI nimekuja kuwa mtumishi wenu, nimekuja kuonyesha njia kwa kile Mh. Rais anachokitaka, anachokitaka Mh. Waziri, mnachokitaka nyie pamoja na wanachokitaka wananchi” Alisema Prof. Makubi.

Aidha, Prof. Makubi amepongeza mafanikio makubwa ambayo Taasisi ya MOI imeyapata toka kuanzishwa kwake mwaka 1996. Pia amepongeza bodi za wadhamini pamoja na wakurugenzi watendaji wote ambao wameshawahi kuitumikia taasisi ya MOI ambapo amesema anathamini na kutambua kazi zao za nyuma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI anayemaliza muda wake Dkt. Respicious Boniface amemshukuru Mh Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan, Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu (Mb) pamoja na viongozi wengine wa Wizara na Serikali kwa kupata nafasi ya kuhudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 6.

“Pia nitoe shukrani za dhati kwa viongozi na watumishi wote wa MOI kwa ushirikiano mlionipa katika kipindi chote naomba ushirikiano huo muendelee kumpa Prof. Makubi kwa manufaa ya Taasisi yetu ya MOI na watanzania wote” Alisema Dkt. Boniface

Kwa upande wao wajumbe wa Menejimenti ya MOI wamemkaribisha Prof. Makubi na kumuahidi ushirikiano wa dhati katika kuboresha huduma za Taasisi ya MOI.

About the Author

You may also like these