KLINIKI JONGEFU GONGO LA MBOTO

Zaidi ya wagonjwa 400 wapata huduma za MOI, Gongo la Mboto

Zaidi ya wagonjwa 400 wamepata huduma za kibingwa za mifupa , Ubongo, Mgongo na mishipa ya fahamu katika kliniki jongefu ya MOI (MOI Mobile Clinic) iliyofanyika leo katika hospitali ya Cardinal Rugambwa , Ukonga.
Kliniki hii ni utekelezaji wa agizo la Serikali ya awamu ya Sita kupitia Wizara ya Afya la kuhakikisha huduma za kibingwa zinasogezwa karibu na wananchi.

Daktari bingwa wa Mifupa MOI Dkt. Bryson Mcharo amesema mwitikio wa wakazi wa Gongo la Mboto umekua mkubwa na wagonjwa wote waliojitokeza wamepata huduma nzuri na kwa wakati.

Dkt. Mcharo ameongeza kwamba asilimia kubwa ya wagonjwa waliojitokeza wanachangamoto za mifupa na maumivu ya Mgongo pamoja na magonjwa mengine.

“Leo tuko hapa katika hospitali ya Cardinal Rugambwa tunatoa huduma kwa wakazi wa Gongo la mboto na maeneo jirani kupitia kliniki yetu pendwa ‘MOI Mobile Clinic’ idadi ya wagonjwa waliojitokeza ni kubwa lakini wote wamehudumiwa” Alisema Dkt Mcharo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Cardinal Rugambwa Dkt Janerose Manyai ameushukuru uongozi wa MOI kwa kushirikiana na hospitali yake kuwahudumia wananchi na kuwapunguzia usumbufu wa kufuata huduma hizo MOI.

Mkazi wa Kitunda Sophia Nestory ameishukuru Taasisi ya MOI kwa kusogeza huduma karibu na hivyo Taasisi nyingine za afya ziige mfano wa MOI kwani sio watanzania wote wanaoweza kufuata huduma hizo MOI.

About the Author

You may also like these