Mtoto wa mwezi mmoja afanyiwa upasuaji katika hospitali ya Rufaa ya kanda Mtwara

Mtoto wa mwezi mmoja (Sinaini Mussa Kalokole) amefanyiwa upasuaji wa kichwa katika hospitali ya rufaa ya kanda Mtwara kwa ushirikiano kati ya Madaktari bingwa wa MOI pamoja na wa hospitali hiyo (SZRH).
Upasuaji huo ni sehemu ya kambi ya matibabu ya siku tano ambayo inaendeshwa na madaktari, wauguzi na wataalamu wa MOI kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali ya rufaa ya kanda ambap hadi sasa zaidi ya wagonjwa 600 wamehudumiwa.

Daktari bingwa wa upasuaji wa Ubongo, Mgongo na mishipa ya fahamu MOI ,Dkt Maxigama Ndossi amesema mtoto huyo alifikishwa katika kliniki na kubainika kuwa na ugonjwa wa kichwa kikubwa ambapo alihitaji kufanyiwa upasuaji ili kumuepusha na madhara yanayoweza kujitokeza kwa kutokupata tiba kwa wakati.

“Leo tuko hapa katika vyumba vya upasuaji vya hospitali ya rufaa ya kanda kusini ambapo tumefanikiwa kwa mara ya kwanza kufanya upasuaji wa kichwa kwa motto wa mwezi mmoja, upasuaji umekwenda salama na mtoto yuko salama kabisa na amepelekwa wodini, tulimuona kliniki na tukabaini anahitaji upasuaji hivyo tumefanikiwa kumfanyia upasuaji wa kichwa” alisema Dkt. Maxigama

Amesema mzazi wa mototo huyo alishakata tama kwani hakuwa na uwezo wa kusafiri kwenda Dar es Salaam kufuata huduma ya upasuaji kwa motto wake.
Dkt. Maxigama ametoa wito kwa wakazi wa mikoa ya kusini kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma katika hospitali ya rufaa ya kanda kusini kwani wataalam wapo na Serikali imeweka vifaa vya kisasa katika hospitali hiyo mpya nay a kisasa.

Taasisi ya MOI imekua ikitekeleza kwa vitendo agizo la Serikali la kuhakikisha huduma zake za kibingwa zinasogezwa karibu na wananchi.

About the Author

You may also like these