MOI YAPOKEA JOPO LA MADAKTARI BINGWA KUTOKA IRELAND

Madaktari bingwa kutoka Ireland wapiga kambi MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili –MOI imepokea jopo la madaktari bingwa wa mifupa wa watoto kutoka Taasisi ya ‘Children Health Ireland Africa’ ambapo wataendesha kambi maalum ya upasuaji kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa MOI kwa siku nne.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface amesema ujio wa madaktari bingwa kutoka Ireland ni sehemu ya mkakati wa MOI wa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za kimataifa ili kuboresha huduma kwa wananachi.

“Leo tumepokea wageni kutoka nchini Ireland ambapo watakua nasi hapa kwa siku nne ambapo watatoa huduma kwa wagonjwa ikiwemo upasuaji kwa watoto 10 wenye viungo vilivyopinda” Alisema Dkt. Boniface

Dkt. Boniface amesema ushirikiano kati ya Taasisi ya MOI na CHIA utajikita katika maeneo ya Mafunzo , kubadilishana watumishi, utafiti, tiba mtandao pamoja na vifaa tiba.

Afisa uendeshaji Mkuu wa Shirika la ‘Children Health Ireland Africa’ Bw. Joe Gannon amesema ni heshima kubwa kupata fursa ya kushirikiana na hospitali ya MOI ili kuangalia namna bora ya kuboresha huduma kwa watoto.

Kwaupande wake Mkurugenzi wa tiba wa Taasisi hiyo ya CHIA Dkt. Paula Llelly amesema ushirikiano kati ya Taasisi yake na MOI utakua na manufaa makubwa kwa pande zote mbili ambapo wanufaika wakubwa watakuwa wagonjwa.

Katika kutekeleza kwa vitendo agizo la Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mh Rais Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi, Taasisi ya MOI imekua ikianzisha ushirikiano na Taasisi mbalimbali za kimataifa ili kuboresha huduma zake kwa watanzania na kumaliza rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

About the Author

You may also like these