ZAIDI YA WAGONJWA 10 WAPANDIKIZWA NYONGA NA GOTI BANDIA ZANZIBAR

Zaidi ya wagonjwa 10 wapandikizwa Nyonga na goti bandia Zanzibar

Na Mwandishi wetu-MOI

Taasisi ya tiba ya Mifupa Muhimbili MOI kwa kushirikiana na hospitali ya rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar zimeendesha kambi maalum ya upasuaji wa kupandikiza goti na nyonga bandia ambapo zaidi ya wagonjwa 10 wamefanyiwa upasuaji.

Kambi hiyo imefanyika ikiwa ni mkakati wa MOI na hospitali ya Mnazi Mmoja wa kuhakikisha huduma za kibingwa za mifupa hususani za upandikizaji wa nyonga na goti bandia zinasogezwa karibu na wakazi wa Tanzania visiwani ili kuwaondolea  adha ya kufuata huduma hizo nje ya Zanzibar.

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui ametoa pongezi kwa uongozi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa kuamua kushirikiana na MOI kuendesha kambi ya upasuaji ambayo ina tija kubwa kwa wananchi hususani wale wenye uhitaji wa kufanyiwa upasuaji wa Nyonga na goti.

“Niwashukuru sana menejimenti ya Mnazi Mmoja pamoja na MOI kwa ushirikiano huu, pia niwapongeze MOI kwa kukubali kuja hapa kufanya kazi hii ya mfano kabisa, sisi Wizara ya afya huwa tunapeleka wagonjwa kutibiwa MOI na wagonjwa wetu huwa wanatibiwa vizuri sana kule MOI lakini hatuna uwezo wa kupeleka watu wote MOI hivyo kambi hii itasaidia wagonjwa wote kuapata huduma hapa” Alisema Mhe. Mazrui.

Mhe. Mazrui ameagiza Taasisi ya MOI pamoja na Hospitali ya Mnazi mmoja  ziingie mkataba wa ushirikiano ili kambi hizi ziwe na muendelezo kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Dkt.Muhiddin Mahmoud amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe Dkt Hussein Mwinyi , Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui kwa usimamizi imara kwenye sekta ya Afya.

Aidha, Dkt. Muhiddin amemshukuru Mkurugenzi Mtandaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface kwa kuridhia kuanzisha ushirikiano na hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar pamoja na kutuma jopo la wataalam 14 kutoa huduma kwa wananchi.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Anthony Assey amesema Taasisi ya MOI imekua ikitekeleza kwa vitendo agizo la Serikali la kuhakikisha huduma za kibingwa za MOI zinasogezwa karibu na wananchi ambapo kwa sasa huduma hizo zinapatikana katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuwapunguzi wananchi usumbufu wa kufuata huduma mbali.

About the Author

You may also like these