70% YA MAJERUHI WA AJALI ZA BARABARANI

70% ya majeruhi wa ajali za barabarani wanaopokelewa MOI wanatokana na ajali za bodaboda

Na Mwandishi wetu – MOI

Naibu katibu Mkuu wa wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalage amefanya ziara katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili MOI kwa lengo la kukagua hali ya utoaji huduma pamoja na kufanya kikao na menejimenti .

Katika ziara hiyo Dkt.Shekalage ametembelea maeneo mbalimbali ya huduma ikiwemo  ICU, HDU, wodi za kawaida na kulipia pamoja na idara ya Radiolojia.

Dkt. Shekalage amesema asilimia 70% ya majeruhi wa ajali za barabarani wanaopokelewa MOI wanataokana na ajali za pikipiki (Bodaboda) hivyo ni muhimu mkutano na wadau ufanyike ili kujadiliana namna bora ya kukabiliana na changamoto hiyo.

“Natoa wito kwa Taasisi ya MOI kuitisha mkutano na wadau ikiwemo jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani pamoja na wadau wengine  ili kuangalia namna bora ya kukabiliana na ongezekola majeruhi wanaotokana na ajali barabarani hususani bodaboda “Alisema Dkt Shekalage

Pia, Dkt. Shekalage amesema asilimia 30-40 ya wagonjwa wanaohudumiwa MOI wangeweza kuhudumiwa katika hospitali za mikoa na wilaya hivyo ni muhimu MOI ikaendelea kuzijengea uwezo hospitali hizo ili kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika MOI kupata huduma.

Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Wizara ya Afya Dkt. Pius Gerald amepongeza kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Taasisi ya MOI na kutoa wito kwa watumishi wa MOI kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu zilizopo.

Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amemshukuru Naibu katiku mkuu Wizara ya Afya kwa kufanya ziara MOI ili kuangalia hali ya utoaji huduma pamoja na kukutana na menejimenti ili kujadiliana namna bora ya kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi.

Dkt. Boniface ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa.

About the Author

You may also like these