MADAKTARI BINGWA KUTOKA AUSTRIA, CZECH, MOI WAENDESHA KAMBI MAALUM YA UPASUAJI

Madaktari bingwa kutoka Austria, Czech, MOI waendesha kambi maalum ya upasuaji

Na Mwandishi wetu – MOI

Madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo kutoka chuo kikuu cha Innsburck Austria , Chuo kikuu cha             Charles Czech kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa MOI wameendesha kambi maalum kwa siku tano ya upasuaji mgumu wa kuondoa uvimbe uliopo chini ya ubongo (Skull base) ambapo wagonjwa waliohudumiwa wangelazimika  kufuata huduma hiyo nje ya nchi.

Katika kambi hiyo maalum, zaidi ya wagonjwa 5 wamefanyiwa upasuaji ambapo upasuaji kwa mgonjwa mmoja hutumia muda wa saa 8 hadi 10.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema hii ni sehemu ya mkakati wa Taasisi ya MOI wa kutekeleza kwa vitendo agizo la Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mh Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha huduma zote za kibingwa zinapatikana hapa nchini.

“Leo tunahitimisha kambi maalum ya upasuaji wa ubongo ambayo tumeshirikiana na wenzetu kutoka Austria na Czech, lengo la kambi hii ni kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wetu ili waweze kutoa huduma hizi hapa nchini, naamini wataalamu wetu wamepata mbinu za kisasa za upasuaji huu mgumu wa kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo na hivyo wataendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wetu hapa nchini.” Alisema Dkt. Boniface

Aidha, Daktari bingwa kutoka hospitali ya Innsburck Austria Dkt. Priv Doz amesema ni heshima kubwa kupata nafasi ya kubadilishana ujuzi na wataalamu wa MOI kwani pamoja na kuleta ujuzi mpya wao pia kuna mbinu ambazo wanajifunza kutoka kwa madaktari bingwa wa MOI.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa huduma za upasuaji wa ubongo ,mgongo na mishipa ya fahamu MOI, Dkt Lemery Mchome amesema kambi hii maalum imekua na tija kubwa kwa wataalamu wa MOI kwani mbinu walizopata zitasaidia kuhudumia wagonjwa ambao wamekua wakilazimika kufuata huduma hizo nje ya nchi.

About the Author

You may also like these