Watumishi MOI wahimizwa kuongeza mbinu za huduma bora kwa wateja.

Na Mwandishi Wetu- MOI Jumanne 26 Septemba 2023.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Prof. Abel Makubi amewahimiza wafanyakazi wa taasisi hiyo kuongeza mbinu za huduma bora kwa wateja wao kwa kutoa huduma kwa wakati, lugha nzuri na kushirikiana kwa pamoja ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Prof. Makubi ameyasema hayo leo Septemba 26, 2023 wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo ya huduma kwa wateja yanayofanyika MOI kwa siku mbili yenye lengo la kuboresha utoaji huduma na kukidhi matarajio ya wateja.

Amesema ili kufikia lengo la taasisi ya MOI kutoa huduma zenye ubora wa kimataifa ni lazima huduma kwa wateja ziendelee kuboreshwa kupitia mafunzo mbalimbali ya ndani yanayotolewa na taasisi hiyo.

“Suala la huduma kwa wateja ni la kila mfanyakazi wa MOI hivyo tufanye kazi kwa umoja na ushirikiano, pindi ukimuona mteja katika eneo lako la kazi mpokee kwa kumkaribisha na muelekeze sehemu husika kwa haraka, lugha nzuri na kutatua kero za wagonjwa kwa wakati ni nyenzo huhimu ili huduma zetu ziwe za kimataifa…

“Kipaumbele cha Wizara ya Afya inayoongozwa na Mh. Ummy Mwalimu (Mb) ni uboreshaji wa huduma kwa wateja, niwapongeze wafanyakazi wa MOI kwa kuendelea kuboresha huduma kwa wateja katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la usafi na ulinzi pia niendelee kuwakumbusha kuwa na sense of ownership katika maeneo yetu ya kazi” Amesema Prof. Makubi.

Amewashukuru NMB kwa kukubali kuendesha mafunzo hayo kwa kushirikiana na Menejimenti ya MOI pia amewashukuru wafanyakazi wa MOI kwa kutenga muda wao na kushiriki hayo mafunzo kwa kuamini bado kila mmoja anahitaji kuendelea kuboresha huduma kwa kuwa na huruma, uvumilivu na upendo katika eneo lake.

Kwa upande wake Mwakilishi wa huduma kwa wateja kutoka benki ya NMB, Benson Moshi amesema lengo la mafunzo hayo ni kukumbushana umuhimu wa huduma kwa wateja kwenye uboreshaji wa huduma za taasisi kwa wananchi ambapo utoaji wa huduma hizo unaanzia ndani ya taasisi.

About the Author

You may also like these