Viongozi MOI wahimizwa kuboresha mawasiliano na mrejesho ili kulete mabadiliko chanya kwa Taasisi.

Na Abdallah Nassoro-MOI

Wakurugenzi na Mameneja wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wameshauriwa kuboresha mbinu za mawasiliano na mrejesho(feedback) baina yao na watendaji wao wa chini pamoja na wagonjwa ili kuiwezesha taasisi hiyo kufikia malengo yake ya kuwa kinara katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa barani Afrika.

Ushauri huo umetolewa leo Januari, 19, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi wakati alipokuwa anawasilisha mada ya dhana uongozi, na kusisitiza kuwa ili taasisi yoyote iweze kufanikiwa ni lazima kuwapo kwa mawasiliano mazuri baina ya viongozi na watendaji wao wa chini pamoja na wateja.

“Mawasiliano na mrejesho ni muhimu kati ya sisi, tunaowaongoza na tunaowatibu , kama hatuwezi kuwasiliana vizuri sisi wenyewe vipi huko kwa wagonjwa wetu, wanapata mrejesho kweli?…MOI inahitaji kusonga mbele, inahitaji maendeleo ili kuyafikia hayo maendeleo ni lazima tuanze leo kuboresha mfumo wa mawasiliano yetu” amesema Prof. Makubi na kuongeza kuwa

“Kiongozi ni lazima uwe na uwezo wa kuleta mabadiliko katika taasisi na kama huwezi kuleta mabadiliko hata ndani ya familia yako, inabidi ujitathimini ”

Amefafanua kuwa lengo la kiongozi ni kuonesha njia katika kuyapatia majibu changamoto zinazowakabili, akitolea mfano wa changamoto ya kifedha na utoaji wa huduma bora ambazo kwa sasa taasisi ya MOI inakabiliwa nayo zinahitaji ubunifu, ushirikishwaji na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kukabiliana nazo.

“Ni lazima kiongozi ukubali kujifunza ili ulete mabadiliko, leteni mabadiliko kwenye usimamizi, shirikisheni wa chini yenu, watieni nguvu wa chini yenu ili kwa pamoja tuweze kufikia lengo”

Kwa upande wake Mkufunzi wa Masuala ya uongozi na huduma bora kwa wateja Bw. John Kasembo amewakumbusha viongozi hao mambo matatu ya kuzingatia ili kufikia malengo kuwa ni pamoja na kujua unachokihitaji, kufanya maamuzi na kutekeleza mipango uliyojiwekea.

Viongozi wa taasisi ya MOI wapo katika mafunzo ya siku nne ya uwongoji ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya kuiboresha MOI katika utoaji huduma bora kwa Wananchi.

About the Author

You may also like these