Mafunzo ya kimkakati ya uongozi kuchochea mabadiliko chanya kwa huduma za wagonjwa MOI

Na Stanley Mwalongo- MOI

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Prof. Abel Makubi amesisitiza mafunzo ya kimkakati ya uongozi yawe chachu ya kuchochea mabadiliko ya kifikra, mitazamo, matendo na tabia za viongozi na watumishi wote wa MOI ili kuboresha zaidi huduma za tiba kwa wagonjwa.

Prof. Makubi ameyasema hayo leo Januari 20, 2024 katika hoteli ya APC Bunju A, Dar es Salaam alipokuwa anahitimisha mafunzo hayo kwa kundi la pili la viongozi wa Taasisi ya MOI.

“Mafunzo haya yatakuwa na maana kubwa kama tutaenda kubadilika, kama umeweza kuhudhuria siku mbili na ukashindwa kubadilika basi mafunzo haya hayatakuwa na maana kubwa kwetu. Kwahiyo nasisitiza haya mafunzo yachochee mabadiliko katika fikra, mtazamo na tabia zetu, matendo na namna bora ya kuwaongoza wenzetu na kutatua changamoto za Taasisi ya MOI” amesema Prof. Makubi

Prof. Makubi amesema ili Taasisi iweze kusonga mbele ni lazima tushirikishane pamoja, tutumie vipaji vya kila mtu, tukubali nawazo mbadala , tuwajibike , tusimamie maadiili na kuboresha mawasiliano na tabia ya kutoa mrejesho kwa viongozi wako wanaokupa maelekezo, wafanyakazi na watumishi waliopo chini yetu na wananchi ambao tunawahudumia kila siku .

Aidha Mkurugenzi Mtendaji huyo amewaomba viongozi hao wayashushe mafunzo hayo kwa watumishi waliopo chini yao na kwenye idara zao ili wabadilike kwa ujumla wetu.

Kwa upande wake Mtaalam wa Masuala ya Uongozi na Utawala Dkt. Daniel Muganyiza amesema kiongozi mzuri ni yule anayeweka malengo yanayoendana na dira ya taasisi na anahakikisha anayafikia katika utekelezaji wake.

About the Author

You may also like these