Huduma EMD

Watumishi Kitengo cha dharura MOI wahimizwa kutoa mrejesho kwa ndugu wa wagonjwa ndani ya nusu saa

Na Mwandishi Wetu MOI, Jumapili Oktoba 15, 2023

Wajumbe wa Menejimenti ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) leo Oktoba 15, 2023 wamefanya ukaguzi katika maeneo mbalinbali ya kutolea huduma kwa lengo la kuangalia changamoto , kusikiliza kero, kuwajulia hali wagonjwa pamoja na kupokea maoni.

Wajumbe hao wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Abel Makubi wametembelea kitengo cha dharura, wodini, mradi wa mashine ya kipimo cha CT SCAN ,MRI na eneo la kusubiria wagonjwa kitengo cha dharura .

Katika kitengo cha dharura Prof. Makubi amewaomba watumishi wa kitengo hicho kufanya kazi kwa pamoja kwa kuzingatia vigezo (SOP) na kutoa mrejesho kwa wateja, ndani ya nusu saa baada ya mgonjwa kufikishwa katika kitengo hicho.

“Wagonjwa au ndugu zao wapewe mrejesho ndani ya nusu saa tangu kufikishwa hapa katika kitengo cha dharura…ni jukumu letu kutoa mrejesho hata kwa hospiali za pembezoni ambazo waliwapa rufaa wagonjwa kuja MOI, ni lazima tuwajulishe hali ya maendeleo ya huyo mgonjwa” amesema Prof. Makubi

Akizungumzia mradi wa ujenzi na usimikaji wa mashine mpya ya MRI na CT Scan Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema “MRI na CT Scan mpya ya pili zinatakiwa kuanza kazi mapema mwezi wa November kama ilivyopangwa ili kuondoa kero za Wananchi kusubiri huduma muda mrefu.

Aidha wajumbe hao wameadhimia kufanyika kwa maboresho makubwa katika kitengo hicho ili kutoa huduma bora kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

About the Author

You may also like these