Watoto sita wenye mtindio wa ubongo wafanyiwa upasuaji MOI

Na Mwandishi Wetu-MOI, Jumamosi Agosti, 26, 2023

Madaktari bingwa wa tiba ya mifupa na viungo kwa watoto kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na wataalam kutoka nchini Uturuki wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji watoto Sita wenye ulemavu wa mifupa na viungo uliosababishwa na mtindio wa ubongo .

Mratibu wa kongamano la kitaaluma la kubadilishana uzoefu wa tiba ya mifupa na viungo kwa watoto kutoka MOI Dkt. Bryson Mcharo amesema leo kwamba upasuaji huo umefanyika kwa mafanikio makubwa chini ya usimamizi wa Pro. Mahereem Inan na Pro. Murat Oto kutoka nchini Uturuki.

“Wenzetu wamekuwa na teknolojia bora ya kufanya upasuaji wa kutibu ulemavu wa mifupa na viungo unaosababishwa na mtindio wa ubongo kwa watoto kwa watoto, mtoto mmoja anafanyiwa orepesheni zaidi ya moja, mtoto mmoja anaweza kuwa na sehemu mbili hadi tatu za upasuaji na zote zinatakiwa kufanyika kwa wakati mmoja” amesema Dkt. Mcharo

“Leo tumewafanyia upasuaji watoto Sita, ambapo kila mmoja amefanyiwa si chini ya operesheni mbili hivyo ni kama operesheni 12 kwa siku… hii yote ni katika kutekeleza dhima ya Wizara ya Afya ya kutoa huduma bora kwa kila Mtanzania …Nawashukuru wenzetu wa Uturuki kwa kubadilishana nasi uzoefu wao, kwa sasa tuna uwezo wa kutoa huduma bora kama wenzetu wa Uingereza na Marekani” amesema Dkt. Mcharo

Kwa upande wake Prof. Inan ameushukuru uongozi wa MOI kwa ushirikiano na kuahidi kuwa katika kongamano la mwaka ujao watapanua wigo zaidi wa kuwahudumia wangojwa na kwamba hiyo ni hatua muhimu ya kubadilishana uzoefu.

“Tumejifunza mengi kupitia operesheni hizi sita, mwaka ujao tutaongeza wigo wa kuwahudumia wagonjwa wengi wakati wa kongamano, tunawashukuru MOI kwa ukarimu wao” amesema Prof. Inan

About the Author

You may also like these