Waelezeni wagonjwa hali zao kiafya

Madaktari wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamehimizwa kuwapa wagonjwa na ndugu wanaowauguza taarifa zinazohusu matatizo ya kiafya yanayowakabili wagonjwa baada ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu stahiki ili kuondoa sintofahamu kwa wagonjwa juu ya mwenendo wa afya zao
Hii inaenda sambamba na utoaji wa huduma bora katika muda mfupi (TAT) ambayo ni sera ya kimkakati ya Wizara ya Afya

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt.Lemeri Mchome ametoa rai hiyo Agosti 21, 2023 wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waajiriwa wapya wa taasisi hiyo yanayoendela katika ukumbi wa MOI.

Dkt.Lemeri Mchome alisema mgonjwa ana haki ya kufahamu hali halisi ya maradhi yanayomkabili na mnyororo wa matibabu anaopaswa kufuata ili kumtibia tatizo hilo.

“Wapeni wagonjwa taarifa kuhusiana na hali zao za kiafya na matibabu yanaondelea na wategemee nini kutoka matibabu hayo, utamkuta mgonjwa hajui hata anachoumwa, hii sio sawa…ni haki yake mgonjwa kujua kinachomsumbua na mnyororo wa matibabu yake…tuwajibike kuleta matokeo chanya ya taasisi yetu” alisema Dkt. Mchome

Alifafanua kuwa “Tunafanya kazi kwa masilahi ya umma na kutoa huduma ile inayotegemewa na wananchi wenzetu, sisi ni watumishi siyo mabosi, utumishi ni kutumika, mgonjwa akifika kwako mpe huduma bora. Hakikisha unakuwa sehemu ya kuleta ufumbuzi kwa matatizo ya wagonjwa na sio kuwaongezea machungu na usumbufu. Tunahitaji kuonyesha uwajibikaji unaoleta matokeo chanya. Karibuni sana katika utumishi wa umma

Awali Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Orest Mushi alisema mafunzo hayo yanalengo la kuwajengea uwezo wa waajiriwa wapya kujua sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

“Mafunzo haya ni muhimu sana kwenu kwasababu yatawajengea uwezo wa kujua sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma” alisema Mushi

Mafunzo hayo yanatolewa na watalam kutoka chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), yakiongonzwa na Mkuu wa Chuo hicho tawi la Dar es Salaam Musa Ligembe ambaye aliwasisitizia waajiriwa hao kuzingatia maadili ya kazi katika utoaji wa huduma zao.

“Maadili ni mtambuka, kila jamii ila maadhili yake lakini sisi kwenye utumishi wa umma tuna maadili yetu ili kulinda misingi ya kazi na hadhi ya utumishi wa umma” alisema ;Ligembe.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Naima Salum aliushukuru uongozi wa MOI kwa mafunzo hayo na kuahidi kuwa watayazingatia ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja wao.

About the Author

You may also like these