Asilimia 60 ya majeruhi wanaoletwa MOI wanatokana na ajali za pikipiki.

Na Mwandishi Wetu, MOI

Asilimia 60 ya majeruhi wa ajali za barabarani wanaopokelewa katika kitengo cha dharura cha Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wanatokana na ajali za bodaboda na bajaji.
Imebainishwa

Daktari bingwa mbobezi wa Mifupa wa Taasisi ya MOI Dkt. Joseph Mwanga alisema hayo Januari, 5, 2024 katika mahojiano maalum kuwa, asimilia 30 ya majeruhi hao wanatokana na ajali za magari na asilimia 10 ajali zingine.

Amesema ajali za pikipiki zinaongoza kwa kusababisha majeruhi huku wanaume wakiwa ndiyo kundi linaloathirika zaidi kwa asilimia 70.

Amebainisha kuwa wengi wa majeruhi hao hupata mivunjiko mikubwa ya mifupa hali inayochangia ukubwa wa gharama za matibabu.

“Unakuta majeruhi kavunjika vibaya sana, mtu huyu atatumia muda mwingi na gharama kubwa kujitibia, wakati nwingine kama sio kifo basi anaweza asirejee katika hali yake ya kawaida…kundi hili la bodabda na bajaji ndilo linaloongoza kwa ajali” amesema Dkt. Mwanga

Ameeleza kuwa miaka 18 iliyopita kitengo cha dharura cha MOI kilikuwa kinapokea majeruhi watatu hadi watano kwa siku, na kwa sasa kitengo hicho kinapokea majeruhi 20 hadi 25 kwa siku.

Ametoa wito kwa waendesha pikipiki kujihurumia wao wenyewe, abiria wao na watumiaji wengine wa barabara ili kupunguza ajali za barabarani.

About the Author

You may also like these