Abdulaziz Seif -MOI
Wanachama wa Klabu ya Simba wamewatembelea watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi walilazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) leo Agosti 2,2024.
Safari hiyo imeambatana na utoaji wa msaada wa mahitaji yakiwemo Sukari, Sabuni, mafuta pamoja na malipo ya matibabu kwa baadhi ya watoto waliolazwa katika wodi ya watoto MOI.
Afisa Ustawi wa Jamii wa MOI, Theofrida Mbilinyi ameishukuru klabu ya Simba pamoja na wanachama wa klabu hiyo kwa msaada huo na kuwaomba kuendelea na moyo wa kuwasaidia watu wenye uhitaji.
“Taasisi ya MOI inatoa shukrani kwa wanachama wote wa simba kwa msaada huu kwani utasaidia kwenye matibabu yao pamoja na kuwapa MOI, pia msaada huu ni sehemu ya kumsapoti Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ambae ameshachangia matibabu ya watoto 100”
Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Simba, Issa Masoud amesema kuwa kuwasaidia watoto hao ni sehemu ya kurudisha fadhila kwa wananchi kuelekea siku ya Simba (Simba day).
“Kuelekea siku ya Simba Day leo tumewatembea watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi ambapo tumewachangia matibabu kwa baadhi ya watoto pamoja na kuwapa mahitaji muhimu, hii ni sehemu ya fadhila kwa watanzania ambao wanatusapoti kila siku”
Kuelekea katika mbio za MOI Marathon, Taasisi ya MOI inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutoa msaada wa matibabu kwa watoto 200 wenye vikubwa na mgongo wazi ambapo Raisi Samia Suluhu Hassan ameshachangia watoto 100.