Na Amani Nsello-MOI
Wauguzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Mubimbili (MOI) wamepewa elimu ya namna ya kujikinga na maumivu ya mgongo na shingo yanayosababishwa na aina ya kazi wanazozifanya.
Elimu hiyo imetolewa mapema jana Jumatano Septemba 04, 2024 katika ukumbi wa jengo la zamani MOI na Wataalamu wa Fiziothelapia wa MOI.
Afisa Fiziotherapia wa MOI, Edson Mpunga amesema maumivu ya mgongo na shingo yanaepukika kwa wahusika kuzingatia njia sahihi za kuinua mzigo ili kulinda afya ya maeneo hayo muhimu ya mwili
“Kabla ya kunyanyua kitu chochote au mzigo unapaswa kuweka plani, au jiulize swali hivi naweza kunyanyua kweli huu mzigo? Lakini kuwa makini na namna unavonyanyua unatakiwa kubalansi uzito, usinyanyue kwa mkono mmoja au upande mmoja utakosa balansi”. amesema Mpunga.
“Mazingira ya kazi yanatakiwa yawe rafiki kwako kwa ajili ya kufanyia kazi na sio wewe ulazimishe mazingira ya kufanyia kazi ili afya ya mgongo na shingo ziendelee kuwa salama”. Amesisitiza Mpunga
Naye Afisa Fiziothelapia mwingine kutoka MOI Emma Badundwa amesema kuwa wauguzi wanatakiwa kufanya kazi kidogo kidogo na kwa awamu hususani kazi za majumbani ikiwa pamoja nakutofua nguo nyingi kwa wakati mmoja.
“Tunapokuwa majumbani mwetu hatutakiwi kufua nguo nyingi kwa wakati mmoja, bora ufue nguo kwa awamu na kidogo kidogo, fua nguo nusu saa pumzika, zingine fua siku inayofuata” Amesema Emma
Idara ya Fiziotherapia kutoka Taasisi ya MOI inatumia wiki ya Fiziotherapia duniani kwa kutoa elimu kwa watumishi wa MOI kutoka idara zote kwa namna bora ya kujikinga na maumivu ya mgongo na shingo
