Na Mwandishi wetu- MOI
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Dkt. Lemeri Mchome akutana na kamati ya tiba ya utalii MOI kwa lengo la kupata mrejesho na kuangalia namna ya kuongeza wateja wa ndani ya nchi na nje ya nchi.
Kliniki ya wagonjwa maalum na wakimatifa MOI ilianzishwa Oktoba 2023, ambapo hadi sasa jumla ya wagonjwa 3,115 wamehudumiwa katika kliniki hiyo ambapo uanzishwaji wa huduma hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha tiba utalii Tanzania.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa Kamati hiyo, Katibu wa kamati hiyo Dkt. Anna Lemunge amesema katika kipindi cha miezi 8 wagonjwa kutoka Mataifa ya Marekani, Ufaransa, China, Korea ya Kusini, Comoro, Congo, Uganda, Malawi, Afrika Kusini, Zimbabwe na Msumbiji wamefika MOI kupata huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.
Dkt. Lemeri ameitaka Kamati hiyo kuongeza msukumo katika utekelezaji wa mikakati mbalimbali ili kuboresha huduma na kuongeza idadi ya wagonjwa wanaokuja kupata huduma MOI.
“Tufanye tathmini ya malengo yetu ya awali, tupime mafanikio na changamoto na tutengeneze malengo mengine na kuboresha mikakati” alisema Dkt Mchome
Aidha, Dkt. Mchome amesema Taasisi ya MOI ina mkakati wa kupanua wigo wa mashirikiano na Taasisi za bima ya Afya Malawi na Serikali ya Congo ili wagonjwa kutoka mataifa hayo waje MOI kupata huduma.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Lemeri ameipongeza Kamati hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali wanakuja kupata huduma za matibabu MOI na kuhakikisha MOI inakuwa kituo cha tiba utalii nchini Tanzania.
