MOI yahimiza bodaboda kujiunga na bima ya afya.

Na Radhia Balozi, MOI

Waendesha Pikipiki maarufu kama bodaboda wamehimizwa kukata bima ya afya ili waweze kupata matibabu kwa urahisi pindi wanapopata ajali za barabrani.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Januari 26, 2024 na Menejimenti ya Taasisi ya tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Prof. Abel Makubi wakati wa kusikiliza maoni, kero, ushauri na pongezi kutoka kwa wateja wao.

Prof. Makubi amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa wa MOI wanatokana na ajali za barabarani hususani za pikipiki zinazotumika kusafirisha abiria.

“Tuwahimize ndugu zetu bodaboda wakate bima ya afya, naamini kipato chao kinaweza kutosheleza kama wakijichanga wakakata bima ili inapotea tatizo waweze kutibiwa kwa urahisi” amesema Prof. Makubi

Ameongeza kuwa “Waliojaa humu ndani (Wodini) asilimia kubwa ni waendesha bodaboda, wengi hawamudu gharama za matibabu sasa wakijiunga na bima ya afya itawasaidia kuwa na akiba ya matibabu ya mbeleni, tuwahimize hawa ndugu zetu”

Pia Mkurugenzi Mtendaji huyo amezungumzia umuhimu wa wananchi kwa ujumla kujiunga na bima ya afya huku akikumbusha jamii kujenga misingi imara ya kusaidiana wakati wa matatizo.

“Kama tunaweza kushirikiana kwenye misiba, tunashirikiana kwenye harusi, sasa kwanini tunashindwa kushirikiana kuwatibu ndugu zetu? amehoji Prof. Makubi na kuongeza kuwa

…ili angalau kuwepo na uendelevu wa hizi huduma, watu wanapaswa kuchangia ili na wengine watibiwe…ila kwa wale wasio kuwa na uwezo kabisa, serikali tuna utaratibu wetu wa kusaidia”

Prof. Makubi amewataka wananchi kutosita kuwaleta wagonjwa MOI na kuondoa dhana ya kujuana ili upata huduma bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Ubongo MOI Dkt. Lemeri Mchome amesema matibabu ya mifupa ni ghali kutokana na mgonjwa kuhitaji kuwekewa vyuma ili kuunga mifupa hata hivyo taasisi hiyo imeendelea kutekeleza sera ya serikali ya kutomuacha mgonjwa bila matibabu kwasababu ya kukosa fedha.

Baadhi ya Wagonjwa wameipongeza MOI kwa huduma bora na kujali wateja, hata hivyo walizungumzia kushindwa kumudu gharama za matibabu kutokana na kipato duni.

“Huduma ni nzuri, wataalam wanatoa ushirikiano, watoto wangu wawili walipata ajali na nilikuwa na akiba ya 40,000 nashukuru tulimuona daktari, majibu yalipotoka hela ya kwenye kipimo iligota” amesema Happy Mlokozi

“Natoa shukurani kwa uongozi wa MOI, kinaja wangu alipotea nikawa sijui aliko nilikuwa na sitofahamu, jana wataalam wa MOI walikuja nyumbani kunitaarifu kuwa mwanangu amelazwa MOI na waliomleta hawajulikani, mishipa ya imekakamaa na nimeruhusiwa niondoke leo” amesema Tija Nassoro

About the Author

You may also like these