Na Abdallah Nassoro-MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inatarajia kuanza matibabu kwa njia ya teknolojia ya kisasa ya kutumia roboti na akili bandıa (artificial Intelligence) katika upasuaji ili kuongeza ufanisi wa tiba kwa wagonjwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi amebainisha hayo leo Januari 30, 2024 katika mahojiano maalum na luninga ya Mtandaoni ya Ayo TV na Azam Tv ambapo amefafanua kuwa matumizi ya akili bandia (artificial intelligence) hayaepukiki katika zama za ukuaji wa sayansi na teknolojia.
“Tunafikiria kuanza kutumia tiba ya kisasa ya kutumia roboti, matumizi ya akili bandia (artificial intelligence) ni muhimu ili kuongeza ufanisi wa operesheni zetu…kwasasa timu inafanya tathimini (assessment), tunaamini ndani ya miaka mitatu ijayo tutaanza kutumia teknolojia hii” amesema Prof. Makubi na kuongeza kuwa
“Baada ya kuanza kufanya kazi teknolojia hii ambayo maeneo mengine imeanza kutumika, tunaamini kuwa baada ya kuanza kwa huduma hii asilimia 99 hawataenda nje ya nchi kwa matibabu tena”
Akizingumzia uboreshaji wa huduma uliofanywa katika taasisi hiyo kwa mwaka 2023 Prof. Makubi amesema eneo la huduma bora kwa wateja limepewa kipaumbele kwa lengo la kuwafanya watoa huduma wawe na lugha na mapokezi mazuri kwa wateja.
“Tumefanikiwa kiasi katika kubadili mtazamo kuwa hospitali za umma haziwezi kuwa na huduma bora kwa mteja (customer care), kila mtoa huduma ameguswa na elimu hiyo na kwasasa hali ni inaanza kubadilika ” amesema
Amefafanua kuwa “Lugha ya madaktari na wahudumu wengine imeboreshwa, kupita kundi letu la WhatsApp tunapokea maoni, sanduku la maoni na uwepo wa redio upepo vyote vimesaidia kuboresha utoaji wa huduma”
Sambamba na hilo MOI imefungua kliniki mpya ya wagonjwa maalum na wa Kimataifa, pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kuchunguza magonjwa kwa lengo la kutoa huduma bora zaidi za mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu Afrika.
”Naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Afya kwa uwekezaji mkubwa kwenye kuboresha huduma za hapa MOI” amesema Prof Makubi.