MOI kuijengea uwezo hospitalii ya Msoga- Chalinze kutoa huduma za dharura za mifupa n ajali .


Na Abdallah Nassoro-MSOGA

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwan Kikwete ameiomba Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kushirikiana na hospitali ya Msoga-Chalinze kuwajengea uwezo wa kiujuzi madaktari wa hospitali hiyo ili waweze kutoa huduma bora za dharura kwa majeruhi wa ajali.

Rai hiyo ameitoa leo Juni, 16, 2024 wakati wa ufungaji wa kambi ya matibabu ya siku tatu ya kibingwa na kibobezi katika hospitali ya Msoga-Challnze.

“Hospitali hii ya Msoga imekaa kati ya barabara kuu mbili, ile iendayo Tanga na ile iendayo iringa na ukiacha Hospitali ya Tumbi na Korogwe na ile ya Morogoro, hamna hospitali nyingine hapa katikati yenye uwezo wa kutoa huduma timilifu za dharura hata matibabu ya awali kwa majeruhi wanaopata ajali katika eneo hili kubwa sana na kupelekea watu wengi kupoteza uhai kwa kukosa matibabu ya dharura kwa wakati…
ajali ikitokea katika ukanda huu sehemu karibu ya kupata huduma za dharura ni Tumbi, hivyo tuliamua kujenga hapa ili kiwe kituo cha msaada wa dharura kwa majeruhi wa mifupa, ubongo na mifumo mingine inayotokana na ajali” amesema Naibu Waziri Ridhiwan

Ameongeza kuwa “MOI ninyi ndiyo wenye mamlaka ya kutibu mifupa na ubongo hapa nchini, niwaombe basi mshirikiane na hawa wataalam wetu muwajengee uwezo ili waweze kutoa matibabu katika kiwango cha kuridhisha, ili kesi ndogondogo zitibiwe hapa”

Amesisitiza kuwa mashirikiano haya yawe ya kudumu na kuomba aletewe taarifa ya vifaa vinavyohitajika ili mamlaka ziweze kuhakikisha huduma hii ya matibabu yanayohusu mifupa, viungo, mgongo na ubongo yanaanza hospitalini hapo.

Naibu waziri huyo ameahidi kuendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati karibu na maeneo wanayoishi ili kuondoa usumbufu na kuokoa vifo vinavyozuilika. Pia amesisitiza umuhimu wa wananhi kupewa elimu ya afya katika nyanja zote ikiwemo kufika hospitali mapema na kupata ushauri wa kitabibu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Lemeri Mchome amesema taasisi yake ipo tayari kuwajengea uwezo wataalam hao ili kuinua hali ya utoaji wa huduma za dharura hospitalini hapo.

“Tunatambua kuwa hospitali hii ipo kandokando ya barabara kuu ya Dar es Salaam Morogoro na Tanga na ni eneo la ajali nyingi zinatokea hivyo kwa niaba ya Taasisi ya MOI tupo tayari kushirikiana kuwajengea uwezo wataalam wa hapa ili waweze kutoa huduma bora za dharura” amesema Lemeri

Ameongeza kuwa “Katika kambi hii wagonjwa 217 wa mifupa, ubongo, mishifapa ya fahamu na Fiziotherapia wamepatiwa matibau ya kibingwa, wengi wao wakiwa wanawake kwa asilimia 65, wanaume asilimia 21 na watoto asilimia 14”

Amesema kambi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya MOI Marathon inayotarajia kufanyiika Juni, 30, 2024 yenye lengo la kusaidia matibabu ya watoto 100 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi ambapo Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

About the Author

You may also like these