Na Abdallah Nassoro-MOI
Simanzi na pongezi zilitawala ndivyo unavyoweza kusema wakati wa hafla fupi ya Menejimeti na wafanyakazi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) walipoagana na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wake Prof. Abel Makubi ambaye ameteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Makao Makuu ya Nchi jijini Dodoma.
Katika hafla hiyo iliyofanyika leo Juni, 7, 2024 katika ukumbi wa MOI Mpya wajumbe wa Menejimenti kwa niaba ya wafanyakazi walishindwa kuzuia hisia zao za huzuni kwa uhamisho wa kiongozi wao ambaye ndani ya miezi 11 ya uongozi wake ameleta mabadiliko makubwa katika taasisi hiyo, hata hivyo hawakusita kumpongeza.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Mifupa Dkt. Antony Assey kwa niaba ya wafanyakazi amemshukuru Prof. Makubi kwa uongozi wake mahiri na kufanikisha mageuzi makubwa ndani ya kipindi cha miezi 11.
“Sisi kama menejimenti tunakupongeza kwa uongozi wako mahiri uliojikita katika ushirikishwaji na utatuzi wa matatizo yetu kwa kutumia rasilimali tulizonazo, nikuhakikishie tutaendeleza yale yote mema uliyoyaanzisha” amesema Dkt. Antony
Kwa upande wake Dkt. Asha Abdullah Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi amesema “Nilishtushwa na taarifa za uhamisho lakini hakuna jinsi, lakini pia nampongeza kwa kuaminiwa kwa mara nyingine na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan … ninachoahidi ni kuendeleza mema yote uliyotuachia”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa MOI, Orest Mushi amesema taasisi ya MOI itaendelea kudumisha misingi imara ya kuboresha huduma na uwajibikaji ili kumuenzi kiongozi huyo.
“Kuondoka kwako ni utumishi wa umma, mtumishi wa umma anaweza kuhamishwa muda wowote, na yote ni katika kuwahudumia Watanzania…sisi kurugenzi saidizi tunasema asante”
Naye Dkt. Joel Bwemelo Meneja Utafiti, Machapisho na Mafunzo amesema uongozi wa Prof. Makubi ni kuigwa kwa kuitejkeleza kwa vitendo dhana ya ushirikishwaji katika kutatua matatizo ya taasisi na wafanyakazi.
Kwa upande mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi TUGHE tawi la MOI, Privatus Masula amempongeza Prof. Makubi kwa kuboresha maslahi ya watumishi na kuongeza ari ya uwajibikaji na kutoa huduma bora kwa wateja.
Prof. Makubi ametumia fursa hiyo kuwashukuru wafanyakazi wa MOI kwa kuonesha ushirikiano na kufanikisha kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kwamba ni jukumu lao kuendeleza Ari hiyo.
“Binafsi naomba niwashukuru kwa kunipokea na kunikubali, Muendeleze mazuri hasahasa ubora wa huduma hilo ndiyo kipaumbele cha wizara na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan…ni jukumu lenu kuendeleza miradi tuliyoianzisha” amesema Prof. Makubi