Prof. Makubi awaaga wagonjwa MOI

Na Abdallah Nassoro-MOI

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Prof. Abel Makubi amewashukuru wagonjwa na ndugu wa wagonjwa kwa ushirikiano wao katika kipindi cha Miezi 11 aliyohudumu kama kiongozi wa juu wa taasisi hiyo.

Shukrani hizo amezitoa leo Juni, 7, 2024 wakati wa kusikiliza maoni, ushauri, kero, changamoto na pongezi kutoka kwa wateja ambapo ametumia fursa hiyo kuwaaga, baada ya kuteuliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo Makao Makuu ya Nchi Jijini Dodoma.

“Niwashukuru kwa ushirikiano wenu katika kipindi nilichokuwa hapa, niwaombe muendelee kutumia jukwaa hili kutoa maoni yenu…tunajitahidi kuyatatua yale yaliyo chini ya uwezo wetu ili mpate huduma mapema, msiogope kutoa maoni eti ukitoa sijui mgonjwa wako atafanyiwa hivi, hakuna hicho kitu hayo ni mambo ya zamani” amesema Prof. Makubi na kuongeza

“Ni lazima muda wetu tuutumie kuhakikisha hapa MOI ni sehemu ya kupona sio kusababisha kifo, kazi yetu sisi madaktari na wauguzi ni kuchelewesha kifo sio kusababisha kifo, Mwenyezi Mungu ametupa dhamana ya kuchelewesha kifo sio kuzuia kifo…
Muwe huru kama una shida mseme…mimi nimekuja kuwaageni lakini wenzangu bado wapo wataendelea kuwapa huduma bora”

Kwa upande wao wagonjwa na ndugu wa wagonjwa waliipongeza menejimenti ya MOI kwa kuboresha huduma “Nimetoka Moshi, wakati natoka kule waliniambia hivi naweza kupata matibabu kweli MOI?, lakini nilipofika hapa nimepokelewa vizuri na mgonjwa wangu amepatiwa matibabu, kwakweli mimi na watu wa Moshi tunawapongeza sana kwa huduma nzuri” amesema Kimario Mushi

Taasisi ya MOI imejiwekea utaratibu wa kusikiliza maoni, ushauri, kero, changamoto na pongezi kutoka kwa wateja wake kwa njia na mkutano kila siku ya Jumatano na Ijumaa ili kupata mrejesho wa huduma kwa lengo la kuziboresha zaidi.

About the Author

You may also like these