Menejimenti ya MOI yakutana ana kwa ana na wateja kusikiliza maoni, ushauri na changamoto.

Na Mwandishi wetu-MOI, Januari 24, 2024

Menejimenti ya Taasisi ya tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imekutana ana kwa ana na wateja wake kwenye eneo la wazi la kusubiria huduma (Clients’ Lounge) kwa lengo la kupokea kero, maoni, pongezi na ushauri ili kujitazama na kuboresha huduma zake kwa Wananchi .

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi amesema ni muhimu Wananchi kutumia fursa hiyo ya kutoa kero zao ili zitatuliwe moja kwa moja na kuacha utaratibu wa kwenda nje ya mifumo iliyopo au kulalamika nje kwani ni wajibu wa Uongozi kuwafikia wagonjwa/Ndugu na kutatua changamoto zao .

“Kuhusu gharama za matibabu , Manejiment ya MOI imeeleza kuwa kweli tiba za Upasuaji wa Mifupa na Ubongo duniani kote zina gharama kubwa kwa sababu ya gharama kubwa ya vifaa kama vyuma vya kuunganisha mifupa (Implants and Screws) lakini Serikali imekuwa ikisaidia kubeba mzigo huo mkubwa huku Wananchi wakichangia kidogo sana kupitia bima zao au fedha taslimu , na wasio na uwezo kabisa bado wanatibiwa.

“Taasisi ya MOI imekuwa ikitekeleza jukumu la sera ya Misamaha kwani kila mwezi inasamehe millioni 300 kwa ajili ya wananchi wasio na uwezo na makundi ya kisera, hivyo serikali yetu ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dr Samia Suluhu Hassan haiwezi kuwaacha wataabike kwani kipaumbele chetu ni chakuwapatia huduma za tiba kwanza siyo na fedha amesema Prof. Makubi.

Prof Makubi ameongeza kuwa ili huduma hizi ziwe na uendelevu ni vema Wananchi wawe tayari kuchangia kidogo kulingana na uwezo wao kupitia Bima za afya .

“Tuzifanye huduma kuwa endelevu ndio maana tunasisitiza kuwa bima za afya pia muwe washauri kwa wengine kwani matibabu ya Mifupa , Mgongo na Ubongo ni gharama” amesema Prof. Makubi.

Vilevile akizungumzia kuhusu swala la walinzi kutokuwa na lugha nzuri kwa wateja Prof. Makubi amesema Uongozi wa MOI utaendelea kuwapa mafunzo mbalimbali maafisa usalama wake ili waendelee kutoa bora kwa wateja na ya kirafiki.

Kwa upande wao wateja wa MOI walitoa maoni mbalimbali ikiwemo suala la uboreshaji huduma kwa wateja kwa askari na wahudumu wengine, suala la gharama za matibabu pamoja na kufungwa kwa (CCTV Camera) eneo la kusubiria wagonjwa ili kuimarisha usalama wa wagonjwa , ndugu, watumishi na mali.

Prof. Makubi amesema Menejimenti itaendelea kuwapa nafasi Wananchi kila wiki mara mbili kukutana moja kwa moja na kusikiliza maoni na kero zao. Aidha, Wananchi wanaweza kutumia njia za simu, ujumbe mfupi, kupiga, kukutana na viongozi na MOI ‘WhatsApp groups’ katika kushauri au kufikisha maoni yao kwa Menejimenti ya MOI.

About the Author

You may also like these