Na. Majid Abdulkarim, Dodoma
SERIKALI imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 55.9 kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa ajili ya kuboresha huduma za tiba na shughuli za uendeshaji.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Prof. Abel Makubi wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi hiyo ndani ya miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita na Mipango ya mwaka 2023-2024 kwa Waandishi wa Habari kupitia Idara ya Habari MAELEZO.
Mkurugenzi huyo ameitaja mipango ya MOI ni pamoja na kuongeza ubora wa huduma zote ndani ili kukidhi matarajio ya wananchi ndani ya nchi na kufikia viwango vya kimataifa.
Aidha, amesema taasisi hiyo imeanzisha huduma mpya tatu za kibingwa bobezi ambazo zinasababisha rufaa ya kwenda nje nchi ikiwemo Tiba ya baadhi ya Kiharusi kupitia Angio-suite, Tiba ya baadhi ya vifafa kupitia upasuaji na upasuaji wa kiuno kwa njia ya matundu (Hip arthroscopy).
Ameeleza mipango mingine ni ukarabati wa miundombinu ya Hospitali ujenzi mpya miundombinu, ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) ambalo litakuwa na vyumba 30 vya kliniki vya kisasa tofauti na vyumba 7 vilivyopo sasa.
Vile vile, ujenzi wa hospitali ya kisasa ya utengamao, mazoezi ya viongo na upasuaji wa mifupa (Rehabilitation and Spine centre) katika kiwanja cha MOI chenye ukubwa wa hekari 10 kilichopo Mbweni Mpiji Mbweni jijini Dar es salaam.
“Kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana muda wote ambapo zimetengwa shilingi Bilioni mbili kwa mwaka huu kupunguza gharama za upasuaji kwa kununua vifaa moja kwa moja kutoka viwandani”. Amesema Prof .Makubi.
Mipango mingine ni kuendelea kuwapa mafunzo wataalamu ili kuwaongezea ujuzi ambapo wataamu 10 wanapelekwa kwenye mafunzo kupitia mfuko wa mafunzo wa Mama Samia.
Halikadhalika amesema MOI imeendelea kujijengea uwezo watumishi wa Hospitali zingine za Kanda na Mikoa ili kupunguza mrundikano wa wagonjwa MOI na kutoa nafuu ya gharama kwa wananchi.
“Kutoa elimu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ili kupunguza ajali za barabarani na kukabiliana na majeruhi kwa harakaā€¯. Ameongeza Prof. Makubi.
Lakini pia amesema kuwa wataimarisha uwajibikaji na usimamizi kwa viongozi na watumishi ndani ya taasisi, kuendelea kushirikiana na MUHAS, MNH na JKCI ili kuleta ubora wa Huduma kwa wananchi wanao wahudumia.