Na Amani Nsello- MOI
Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inaendelea kuonesha dhamira yake ya kuboresha huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kwa wananchi.
Akifungua wiki hiyo jana Oktoba 06, 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya alieleza kwamba taasisi hiyo inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kuboresha huduma, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la Wagonjwa wa nje (New OPD) litakalorahisisha upatinakanaji wa huduma kwa wagonjwa wa nje.
“Mradi wa jengo jipya la OPD unalenga kupunguza msongamano, kuongeza ufanisi na kutoa huduma kwa mazingira rafiki zaidi Tunataka kila mgonjwa anaefika MOI anafurahia huduma bora za matibabu ya kibingwa na kibobezi” alisema Dkt. Mpoki
Kwa upende wake Bi. Zaituni Bembe, kutoka Kitengo cha Udhibiti Ubora MOI, alisisitiza umuhimu kuwahudumia wagonjwa kwa utu na huruma kama sehemu ya dira na dhamira ya taasisi hiyo.
“Huduma bora inaanza na tabasamu, tunawahudumia wateja wetu kwa upendo, uvumilivu na heshima… Kwa sababu kila mgonjwa anastahili kutunzwa na kupata huduma bora za matibanu” alisema Bi. Zaituni
Wiki hiyo ilianza rasmi jana Oktoba 06, 2025 na itafikia tamati Oktoba 10, 2025 ambapo wataalam wa MOI wanatarajiwa kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wagonjwa na kupokea maoni kwa ajili ya kuboresha huduma katika taasisi hiyo.