Waziri Mhagama aagiza sheria ya uanzishwaji wa taasisi ya MOI kufanyiwa marekebisho

Na Amani Nsello-MOI

Waziri wa Afya Mheshimiwa Jenista Mhagama ameiagiza Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kufanyia marekebisho sheria namba 7 ya mwaka 1996 iliyoanzisha Taasisi hiyo ili iendane na wakati pamoja na mabadiliko ya sayansi ya tiba na teknolojia kwa lengo la kuboresha huduma.

Maagizo hayo yalitolewa jana Jumatano Septemba 11, 2024 katika ziara yake ya kikazi MOI wakati akizungumza na watumishi wa taasisi hiyo, ambapo amesisitiza sheria hiyo inahitaji marekebisho ili kutanua wigo wa wananchi kupata huduma bora za kibingwa na kibobezi nchini.

“Sheria iliyotumika kuanzishwa kwa hii taasisi ni ya muda mrefu sana, Mkurugenzi umesema hapa kuwa imeanzishwa mwaka 1996, ni mbali sana, angalieni namna ya kufanyia marekebisho, nadhani hadi kufikia mwezi wa kumi muwe mmekamilisha mchakato wa haya mabadiliko ya sheria”. amesema Mhe. Mhagama

Aidha Waziri Mhagama amewapongeza madaktari wa MOI kwa kutoa huduma bora za kibingwa na kibobezi kwa wagonjwa hali iliyosababisha kupungua kwa rufaa za wagonjwa wa mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

“Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika vifaa tiba na ujuzi kwa wataalam wetu, umeweza kuboresha huduma za kibingwa na kibobezi, nimekutana na dada hapo kafanyiwa upasuaji wa ubongo mara mbili na sasa yupo ‘super’…miaka mitatu iliyopita mgonjwa kama huyu alitakiwa kupelekwa nje ya nchi…hongereni sana madaktari wetu” amesema Waziri Mhagama

Awali akizungumza katika kikao kazi hicho Kaimu Mkurugenzi wa taasisi ya MOI Dkt. Lemeri Mchome ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zaidi ya bilioni 10 za Kitanzania kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha bilioni 10.8 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje, ambapo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 1,000 kwa siku na litakuwa na vyumba 40 vya kuonea wagonjwa” . amesema Dkt. Lemeri na kuongeza

“Pia tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba ukiachilia mbali rasilimali watu ametoa zaidi ya bilioni 26 ambazo zinatuwezesha sisi kutoa matibabu ya kibingwa na kibobezi ambayo yanatolewa sehemu mbalimbali ulaya na Marekani na Bara la Asia.

Upande wa mifupa zaidi ya asilimia 99 ya magonjwa yote ya mifupa yanatibiwa hapa ndani ya nchi na kwa upande wa ubongo na mishipa ya fahamu zaidi ya asilimia 96 yote yanatibiwa ndani ya nchi na hii ni kwa sababu ya uwekezaji wa serikali ya awamu ya sita.”

About the Author

You may also like these