Na Abdallah Nassoro-MOI
Watumishi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamepatiwa elimu namna ya kuepuka na changamoto ya afya ya akili mahali pa kazi ili kuongeza ufanisi.
Elimu hiyo imetolewa leo Jumatano, Septemba 18, 2024 katika ukumbi wa mikutano uliopo jengo jipya la taasisi ya MOI.
Muwezeshaji wa mafunzo hayo Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Milembe Dkt. Sadiki Mandari amesema kuwa baadhi ya watumishi wa MOI wanapaswa kuepuka matarijio makubwa na matumizi ya pombe kupitiliza.
“Siku hizi tatizo hili la afya ya akili limeota mizizi hususani kwa watumishi wa umma, asubuhi mtumishi kafika ofisini kanuna hata mchana haijafika, usiku kanywa pombe, kabla hajaondoka nyumbani kuja kazini kavurugana na mwenza wake, nawasihi sana matumizi ya pombe sio mazuri kama hujawahi kunywa pombe usinywe ili kulinda afya yako ya akili pia acheni kuwaza matarajio makubwa baada ya kupata kazi (ajira)”. amesema Dkt. Sadiki
Sambamba na hilo Dkt. Sadiki amesema kuwa madeni mengi, umaskini, kuvunjika kwa ndoa, kufilisika, kufukuzwa, kupoteza wazazi, kifo cha mtu wa karibu na kugombana kwa wazazi ni vyanzo vya changamoto ya afya ya akili katika jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Orest Mushi kutoka taasisi ya MOI amesema mafunzo hayo yanalenga kutatua changamoto ya afya ya akili kwa watumishi ili kuongeza ufanisi sehemu ya kazi.
“Mafunzo haya ni muongozo kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuwa watumishi wa umma wapatiwe elimu ya udhibiti wa VVU, UKIMWI, Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza na elimu juu ya Afya ya Akili mahali pa kazi…sisi kama MOI tumelitekeleza hili” amesema Mushi