Na Amani Nsello-MOI
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama (Mb) ameipongeza Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo muhimbili (MOI) kwa kupunguza idadi ya wagonjwa wa mifupa, ubongo na mishipa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Pongezi hizo amezitoa leo Jumatano Septemba 11, 2024 wakati wa ziara yake ya kikazi katika taasisi ya MOI.
“Nimekutana na mgonjwa kashafanyiwa oparesheni ya ubongo mara mbili na yupo vizuri, tumeokoa fedha nyingi ambazo serikali ingezitumia kwa ajili ya matibabu, pia tunapunguza mzigo mkubwa kwa wananchi katika kujisimamia kuhangaika kutafuta tiba hizi ambazo ni za kibobezi nje lakini zinakafanyika ndani”. amesema Mhe. Mhagama
Aidha Waziri Mhagama ameipongeza pia Taasisi ya MOI kwa kutenga siku za Jumatano na Ijumaa kwa ajili ya kusikiliza kero, maoni, mapendekezo na changamoto kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa kwani hiyo ni njia bora ya kupata mrejesho kutoka kwa wagonjwa wanaopatiwa huduma za kimatibabu na kuboresha huduma kwa wateja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya MOI Prof. Charles Mkony amemshukuru Mhe. Rais wa Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuendelea kuijali na kuithamini Taasisi ya MOI kwa kuibua miradi mingi ikiwemo wa mradi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje.
“Sisi wote hapa ni mashahidi miradi inayoendelea hapa MOI ni jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali na kuithamini Taasisi hii kwa kutoa fedha nyingi za miradi ili kuwezesha huduma bora za matibabu…ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje, likikamilika litakuwa suluhisho kwa kupunguza msongamano uliopo wa sasa”. amesema Prof Charles
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI amesema kuwa Taasisi ya MOI imeshaanzisha matibabu ya wagonjwa wa kiharusi na tayari imewezesha baadhi ya wataalam kuhudhuria mafunzo nje ya nchi na kuendesha mafunzo ndani ya nchi kwa kuleta wataalam kutoka mataifa ya nje ili kuwajengea uwezo madaktari bingwa wa taasisi hiyo.
“Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba ukiachilia mbali rasilimali watu ametoa zaidi ya bilioni 26 ambazo zinatuwezesha sisi kutoa matibabu ya kibingwa na kibobezi ambayo yanatolewa sehemu mbalimbali duniani”. Amesema Dkt. Mchome
“Upande wa mifupa zaidi ya asilimia 99 ya magonjwa yote ya mifupa yanatibiwa hapa ndani ya nchi na kwa upande wa ubongo na mishipa ya fahamu zaidi ya asilimia 96 yote yanatibuwa ndani ya nchi na hii ni kwa sababu ya uwekezaji wa serikali ya awamu ya sita.” Ameongezea Dkt. Mchome