Na Abdulaziz Seif-MOI
Watumishi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) leo Mei, 15, 2024 kwa mara ya kwanza wameadhimisha siku ya familia duniani kwa kushiriki katika mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia, Saikolojia na watoto ili kujenga jamii yenye ustawi.
Mwezeshaji wa Mafunzo hayo Afisa Ustawi wa Jamii MOI, Bi.Stellah Kihombo amesema ni vema kwa jamii kujiepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto ikiwa pamoja na unyanyasaji wa kimwili, kingono na kisaikolojia na kuvunja ukimya kwa wahanga ili waweze kupata msaada wa ushauri.
“Epuka ukatili wa kisaikolojia, kuna yale maneno yanayomuathiri mtu kisaikolojia…madhara ya ukatili wa kisaikolojia yanaenda mbali hadi kuathiri ufanisi kazini…sisi kama wanafamilia ya MOI tujiepushe na aina zote za ukatili” amesema Bi.Kihombo na kuongeza
“Tuwekeze kwa watoto wetu ili watusaidie uzeeni, tuwasomeshe na kutimiza mahitaji yao…wanaume pia ni waathirika wa ukatili wa kijinsia, wapo wanaopigwa, wapo wanaonyanyaswa lakini wanaamua kufa na tai shingoni…niwaombe wale wote wenye changamoto za kifamilia wafike ofisini kwetu ili tuwape ushauri”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Bw.Orest Mushi akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MOI amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa watumishi na kutaka yawe endelevu.
“Nikiri kuwa hii ni mara ya kwanza kuadhimisha siku ya familia duniani, hiki kilichofanyika leo ni muhimu sana na naomba kiwe endelevu, ni muhimu kwa watumishi wetu wakafahamu masuala mtambuka kama haya ili kufanikisha azma ya taasisi yetu ya kuboresha huduma, hii MOI mpya basi iwe mpya kwa kila sehemu”
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi Bw.Fidelis Minja amesema kurugenzi yake iliona ni vyema kuadhimisha siku ya familia kwa kukumbusha umuhimu wa kupiga vita ukatili wa kijinsia kwa watoto na saikolojia.
Meneja Ustawi wa Jamii Bw.Juma Almasi amesema ofisi zake zipo wazi kwaajili ya kutoa msaada wa kiushauri kwa watumishi wa MOI kuhusu masuala ya kifamilia na kijamii ili kuboresha ufanisi wa kazi sehemu ya kazi.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Tukubali tofauti zetu kwenye familia, kuimarisha malezi ya watoto”
