Na Abdallah Nassoro-MOI
Menejimenti ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imewashauri wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo kutosubiri siku ya Jumatano na Ijumaa kwa ajili ya kutoa maoni ya changamoto wanazokutananazo wakati wa kupata huduma badala yake wafanye hivyo kupitia kundi la WhatsApp na namba za viongozi ili changamoto zao zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.
Ushauri huo umetolewa leo Jumatano Mei, 15, 2024 na Meneja Rasilimali watu wa MOI, Marry Kayora wakati akihitimisha zoezi la kusikiliza maoni, ushauri, changamoto na pongezi kutoka kwa wateja katika banda la kusubiria wateja MOI mpya.
Amesema ni vema kwa wateja hao kujenga utamaduni wa kuripoti changamoto, kero au malalamiko kwa wakati ili yapatiwe utatuzi kwa haraka bila kuathiri mwenendo wa matibabu.
‘Niwasihi msisubiri katika mkusanyiko huu ndiyo mtoe maoni yenu, tunalo kundi la WhatsApp la huduma kwa wateja, pia tunalo bango la namba za viongozi, unaweza kuwasiliana nao mda wowote na changamoto yako ikatatuliwa” amesema Kayora
Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa MOI Patrick Mvungi amesema utaratibu huo unalenga kupata mrejesho wa huduma wanazotoa kutoka kwa wateja ili menejimenti iweze kuboresha zaidi.
“Niwashukuru kwa pongezi zenu, tumezipokea na zinasaidia kutia moyo na kuongeza hari ya kutoa huduma bora endelevu” amesema Mvungi
Mmoja wa ndugu wa wagonjwa, Salma Amri ameipongeza MOI kwa huduma bora kwa wangonjwa ikiwa sambamba na wahudumu kutoa maelekezo kwa wagonjwa kwa upendo.
Taasisi ya MOI imejiwekea utaratibu wa kusikiliza maoni, ushauri, kero, changamoto na pongezi kutoka kwa wateja wake kwa njia ya moja kwa moja kwa siku za Jumatano na Ijumaa kuanzia saa 5 hadi saa 6 mchana.
