Na Abdallah Nassoro-MOI
Watoto wenye ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kugharamia matibabu ya watoto 100 katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), ambapo pia wamemuomba kuangalia uwezekano wa kuondoa gharama hizo za matibabu ili watoto wengi wenye changamoto hiyo waweze kutibiwa.
Katika risala yao iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel na Johari Idd mwenye ulemavu wa mgongo wazi wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi Duniani, iliyofanyika kitaifa siku ya Oktoba, 25, 2024 katika uwanja wa MUHAS jijini Dar es Salaam ambapo watoto hao wamesema walijisikia faraja kupata msaada huo wa matibabu.
“Sisi watoto wenye ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutugharamia matibabu ya watoto 100.” amesema Johari
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Mollel amesema serikali itaendelea kuwekeza kwenye sekta ya afya ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora ya matibabu ikiwamo watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.
“Tumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika vifaa tiba CT Scan na MRI, vifaa ambavyo vimewezesha watoto hawa kupatiwa matibabu ya kibingwa hapa nchini….na niwaahidi serikali itaendelea kuboresha kwa kuhakikisha vifaa tiba zaidi zinawekezwa katika hospitali zetu” amesema Dkt. Mollel
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MOI Dkt. Nicephorus Rutabasibwa amesema zaidi ya watoto 7,500 huzaliwa na ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi kila mwaka nchini na kati yao watoto 800 pekee ndiyo wanaopatiwa matibabu MOI.
“Inakadiriwa kuwa kila mwaka watoto 7500 huzaliwa wakiwa na tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi, hii inaifanya Tanzania kuwa nchi ya Tatu Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye changamoto hiyo, ikitanguliwana Algeria na Ethiopia” amesema Dkt. Rutabasibwa na kuongeza
“Kuna sababu nyingi zinazochangia mama kujifungua mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi ikiwa pamoja na ukosefu wa madini ya folic acid mwilini hasa ndani ya siku 21-28 tangu mama ashike ujauzito”
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wenye watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi Tanzania (ASBAHT) Ramadhani Mwaluka amesema mbali na changamoto ya gharama za matibabu kwa watoto hao nguvu kubwa inatakiwa kuwekezwa katika kuzuia kwa uhakikisha wanawake walio katika umri wa uzazi wanapata elimu sahihi ya kujikinga.
“Kwa sasa ASBAHT tuna wanachama 12,800 katika mikoa 11 ya Tanzania, ombi letu kwa serikali itangaze matibabu bure kwa watoto wenye matatizo haya ili waweze kujitokeza kwa wingi kupata matibabu tofauti na sasa ambapo gharama zatibabu zimekuwa kikwazo, pia tuwekeze nguvu zaidi katika elimu ya kuzia tatizo” amesema Mwaluka