Na Abdallah Nassoro-MOI
Wafanyakazi wapya wa kitengo cha usafi katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na uaminifu mkubwa huku wakiaswa kujiepusha na vitendo vya wizi ili kuiwezesha taasisi hiyo kutekeleza kwa ufanisi mpango mkakati wake wa kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Wito huo ulitolewa siku ya Alhamisi, Oktoba 24, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi MOI, Fidelis Minja wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa wafanyakazi hao kutoka kampuni ya SITI Retails and General Supplies Ltd ya jijini Dar es Salaam.
“Kuweni waaminifu na wala msikubali mkashawishiwa kuingia katika wizi, tukibaini hilo na sisi tutakukataa…niwaombe sana fanyeni kazi wa bidii na kuzingatia kanuni na taratibu za sehemu ya kazi, shirikianeni katika kufanya kazi ili kuisaidia taasisi kutimiza majukumu yake” alisema Minja na kuongeza kuwa
“Kuweni washirika wazuri wa MOI kufanikisha malengo yake hapa ni hospitali lakini mmepakuta ni pa safi na salama, ni kwasababu waliopo kwa sasa wanatimiza wajibu wao vizuri, hivyo hatutegemei ninyi mfanye chini ya hapo”
Wafanya kazi hao ambao watahudumu katika kitengo cha usafi wanatarajia kuanza kutoa huduma hivi karibuni na kutoa mchango chanya katika kuboresha mazingira ya kutolea huduma kwa wagonjwa