Na Amani Nsello- MOI
Watumishi wapya 28 wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), wamepatiwa mafunzo elekezi ya awali huku wakiaswa kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma na kufanya kazi kwa bidii na weledi.
Mafunzo hayo ya siku tatu, yenye lengo la kuwapa uelewa wa sheria, kanuni, sera na misingi ya Utumishi wa Umma, yameanza leo Alhamisi Oktoba 24, 2024 katika ukumbi wa mikutano uliopo katika taasisi ya MOI.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa MOI, Orest Mushi ambaye amewaasa watumishi hao wapya kufanya kazi kwa bidii na weledi huku wakizingatia maadili ya Utumishi wa Umma.
“Mmebahatika kupata kazi, niwapongeze kwa hilo, lakini kwa sasa nyie ni watumishi wa MOI na mnapaswa kuzingatia maadili yote ya utumishi wa umma na ndiyo muongozo wenu katika kufanya kazi, mnatakiwa mfanye kazi kwa bidii na weledi, mjieupushe na kutoa lugha chafu iwe kazini au majumbani kwenu, rushwa hapa MOI sio mahali pake, epukeni kuomba rushwa”. Amesema Bw. Mushi
Naye, Meneja wa Mafunzo kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania tawi la Dar es Salaam, Fadhili Mtinda amewakumbusha watumishi hao umuhimu wa kujiepusha na rushwa na kutoa huduma bora bila ya upendeleo, pia kuzingatia sheria za utendaji wa kazi serikalini.
“Serikalini kuna miongozo ambayo inamuongoza mtumishi wa umma, kama ile ya kutoa huduma bora bila ya upendeleo, wahudumieni wananchi kwa usawa na mnatakiwa mzingatie sheria zote za utendaji kazi serikalini”. Amesema Bw. Mtinda
Bw. Mtinda pia amewafundisha watumishi hao wapya mfumo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, muundo wake pamoja na mfumo wa mamlaka na madaraka ya serikali.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi amewahimiza watumishi hao wapya kuilinda taswira ya MOI, kwani imejengwa kwa muda mrefu zaidi ya miaka 20 hadi sasa, pia wazingatie maudhui wanayoweka katika mitandao yao ya kijamii, kwani wao ndiyo wameibeba taswira ya taasisi hiyo na kuwa mabalozi wazuri wa MOI.
Mafunzo hayo ya siku tatu yameanza Alhamisi Oktoba 24, 2024 na yatafikia tamati Oktoba 28, 2024 katika taasisi ya MOI