Wajumbe wa kamati ya Bunge ya maendeleo ya jamii Namibia wafurahishwa na huduma za kibingwa zinazotolewa MOI

Na Mwandishi wetu-MOI, 15 June 2023, Dare es Salaam.

Wajumbe wa kamati ya maendeleo ya jamii ya Bunge la Namibia leo wametembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) ili kujifunza na kuona hali ya utoaji huduma ili kuangalia namna bora ya kuanzisha ushirikiano ili wagonjwa kutoka nchini Namibia waje Tanzania kupata huduma.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika Taasisi ya MOI katika vifaa tiba na miundombinu hivyo wagonjwa kutoka Taifa la Namibia wanaweza kuja kupata huduma hapa nchini kwa gharama nafuu.

“Leo tunafuraha kupokea ugeni wa wajumbe wa kamati ya huduma za jamii ya Bunge la Namibia ambao wametembelea Taasisi yetu ya MOI, tumewaeleza na kuwaonyesha huduma na vifaa vya kisasa tulivyonavyo, naamini hii itapelekea wagonjwa kutoka Namibia kuja hapa kupata huduma kibingwa za upasuaji wa Ubongo kwa njia ya matundu, upasuaji wa Mgongo kwa darubini na huduma nyingine nyingi zinazopatikana MOI” Alisema Prof. Makubi.

Prof. Makubi amesema wananchi kutoka mataifa ya Kenya, Comoro, Zambia na Malawi wamekua wakipata huduma hapa MOI hivyo ni muda muafaka wa wagonjwa kutoka nchi ya Namibia kuanza kupata huduma MOI na kuondokana na changamoto ya kufuata huduma hizo nje ya bara la Afrika.

Kwa upande wake Mwenyekitiki wa kamati hiyo Mhe. Julietha Kavetuna ameipongeza Taasisi ya MOI kwa kutoa huduma za kibobezi za mifupa, Ubongo, Mgongo na mishipa ya fahamu zenye ubora wa hali ya juu na hivyo kuwa tegemezi kwa wagonjwa kutoka mataifa jirani.

“Ni heshima kubwa kupata nafasi ya kutembelea hospitali hii ya kisasa ya MOI, tumeona ina miundombinu, vifaa na mashine za kisasa ambazo zimewekezwa na Serikali ya Tanzania, hii inatupa msukumo mkubwa kuangalia namna bora ya kushirikiana ili Tanzania iwe chaguo letu la kwanza kwa wagonjwa wetu kupata matibabu badala ya kuwapeleka nje ya bara la Afrika kwa gharama kubwa” Alisema Mhe Julietha

Awali, Mkurugenzi wa huduma za upasuaji wa Ubongo na Mgongo MOI Dkt. Lemery Mchome aliwaeleza wajumbe wa kamati hiyo kwamba huduma na vifaa vinavyopatikana MOI ni sawa na hospitali zilizopo katika mataifa ya Ulaya na India.

Pamoja na mambo mengine wajumbe wa kamati hiyo wametembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

About the Author

You may also like these